Kigwangalla ajibu matumizi ya Sh2 bilioni kinyume na utaratibu

Wednesday April 8 2020

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amewajibu wanaomsakama katika mitandao ya kijamii wakitaka awajibike  baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania (CAG) kubaini  matumizi ya Sh2.58 bilioni yaliyofanywa na wizara hiyo  nje ya bajeti na kabla ya kupitishwa na Bunge.

Katika majibu yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Dk Kigwangalla amesema haogopi kutumbuliwa, kuwataka wahusika kusubiri muda muafaka wa ripoti hiyo kujadiliwa bungeni ili kujua ukweli na kusisitiza kuwa wakati ukaguzi huo unafanyika alikuwa amelazwa hospitali na ana amini timu ya wizara hiyo ilifuata utaratibu.

Ripoti kuu ya mwaka kuhusu ukaguzi wa taarifa za fedha za Serikali kuu kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2019, ilieleza matumizi ya Sh2.58 bilioni yaliyofanywa na Wizara hiyo nje ya bajeti na kabla ya kupitishwa na Bunge.

Fedha hizo zimetumika kufanikisha kampeni ya Urithi Festival Celebration and Channel maalum ya kutangaza vivutio vya utalii kinyume na taratibu.

 “Nilipitia matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kubaini kiasi cha Sh2.58 bilioni kimetumika kuanzisha chaneli ya Televisioni “Urithi Festival” ili kutangaza vivutio vya utalii,” imeeleza ripoti hiyo.

 

Advertisement

Imeeleza kuwa katika kutambua chanzo ya kugharamia matumizi hayo,  hayakuwa na kifungu cha bajeti kama ilivyopitishwa na Bunge.

 

Imeeleza kuwa fedha hizo zilitolewa katika vifungu vingine vya matumizi ya wizara na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo ambazo ni Tanapa, NCAA, Tawa na TFSA.

 

“Nilijulishwa kuwa bajeti ya Urithi Festival ilipitishwa na menejimenti ya Wizara katika vikao mbalimbali vilivyofanyika,” inaeleza taarifa hiyo,” inaeleza taarifa hiyo ya CAG.

 

Alichokijibu Kigwangalla

 

“Kuna tuhuma nyingi huwa nazipuuza. Kuna vitu vingi huwa naviacha vipite, lakini siyo tuhuma ya kuwa nimekula Sh2.58 bilioni ya umma jamani! Hii ni nzito na huwezi na wala hupaswi kuiacha ipite. Pamoja na maelezo bado kuna mtu anakung’ang’ania tu. Tena bila ushahidi hata kidogo wa wizi,” aliandika waziri huyo.

Dk Meni katika ukurasa wa Dk Kigwangalla aliandika,“Hivi aliyeleta mfumo wa kujiwajibisha unadhani alikuwa mjinga? kuwajibika bila kuwajibishwa ni dalili za ukomavu wa kifikra sasa nakushangaa Dk unaogopa kuachia ngazi ili ukweli ujulikane? Achia ngazi.”

Akijibu hoja hiyo ya kuachia ngazi, Dk Kigwangalla amesema; “Nikiachia ngazi wewe utafaidika na nini? Na niachie ngazi kwa sababu gani? Kosa langu ni nini? Labda tuanzie hapo kwanza. Kuachia ngazi siyo shida sana kwangu, lakini nisaidie hayo majibu hapo kwanza!.”

Mchangiaji mwingine aitwaye Millinga lihoji kuhusu kutumbuliwa kwa waziri huyo ambaye alimjibu kuwa hakuna shida hilo likitokea.

 “Maana nishachoka kujitoa kuwatumikia watu wasio na shukrani kama wewe! unadhani kuwa Waziri ni feva kwangu ama ni fursa kubwa sana kwangu? Hiyo ndiyo shida. Kwangu ni nafasi ya utumishi na ninajitoa sana kuitumikia nchi yangu,” amesema mbunge huyo wa Nzega Vijijini.

Katika ufafanuzi wake, Dk Kigwangalla amesema kifungu cha 11(5) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma 2008 kinampa mamlaka CAG kuchukua hatua kwa ofisa aliyetumia vibaya fedha za umma, na ukurasa wa ripoti unaozunguka mtandaoni, CAG hakuchukua hatua kwa sababu hakuna wizi uliofanyika.

Dk Kigwangalla amesema ripoti za CAG zitajadiliwa Bunge la Februari mwaka 2021  baada ya maafisa masuhuli wote wa wizara kuitwa kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kutoa ufafanuzi. Amesema baada ya hapo  wananchi wataelezwa hoja kwa hoja kupitia Bunge na ukweli hubainika.

“Ripoti ya CAG ni ya kipindi kuishia Juni 30, 2019. Katika kipindi hicho, nilikuwa nimelazwa hospitali na baadaye kupumzika nyumbani kufuatia ajali ya gari nikiwa kazini kuitumikia nchi yangu, na nina hakika menejimenti ya Wizara iliyokuwepo ilifuata taratibu,” amesema.

Advertisement