Kiongozi Chaso aliyekamatwa Udom aachiwa, aomba radhi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Chadema (Chaso) tawi la Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) nchini Tanzania, Henry Mang’era ameachiwa huru kisha kuomba radhi kwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Dodoma. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chaso) wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) nchini Tanzania, Henry Mang’era ameachiwa huru leo Jumatatu Desemba 2, 2019 baada ya kushikiliwa kwa siku tatu na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na siasa ndani ya chuo hicho.

Baada ya kuachiwa, Mang’era aliyekamatwa na polisi tangu Ijumaa iliyopita ya Novemba 29, 2019 na kuachiwa leo Jumatatu, kilifanyika kikao kati yake na uongozi wa Udoma.

Polisi walipokamata walimnyima dhamana mwanafunzi huyo kwa madai ya kuhatarisha usalama chuo hapo kwa kuwashawishi wanafunzi wa mwaka wa kwanza kujiunga na Chadema.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Uhusiano wa Umma na Masoko wa Udom, Prudence Rwehabura amekiri kushikiliwa na polisi lakini si kwa wiki mbili kama ilivyoandikwa kwenye mitandao ya jamii.

Amesema mwanafunzi huyo alikamatwa Ijumaa na kuachiwa leo na baadaye kuwa na mazungumzo na uongozi wa chuo.

Amesema baada ya  mwanafunzi huyo kuonyeshwa sheria ndogo ndogo inayokataza wanafunzi kujishughulisha na siasa ndani ya chuo, alikiri na kumsamehewa.

"Amekiri na kusema kuwa hatarudia tena kosa hilo, uongozi wa chuo umemsamehe. Na amejaza fomu ya kuonyesha hatarudia tena, kwa hiyo hilo limekwisha na anaendelea na masomo yake kama kawaida, amesema.