Kituo cha Tehama kwa nchi za EAC chazinduliwa Tanzania

Friday August 23 2019

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Afrika Mashariki, EAC,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Joyce Ndalichako,

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Joyce Ndalichako amezindua kituo cha umahiri cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Afrika Mashariki kilichoanzishwa katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) jijini Arusha nchini Tanzania.

Uzinduzi huo umefanyika leo Ijumaa Agosti 23,2019 ambapo Waziri Ndalichako amesema kituo hicho kilichofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kinalenga kuwajengea uwezo Watanzania pamoja na wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Amesema kituo hicho kitaleta maendeleo ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili wa masomo ya shahada za uzamili.

Waziri Ndalichako amesema Mwongozo wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu unatambua nafasi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kama nyenzo muhimu katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nyanja mbalimbali yakiwemo masuala ya viwanda, uchumi na maeneo mengine akitolea mfano mifumo ya fedha inayotumia Tehama inavyotumika EAC.

“Teknolojia na  ubunifu kwa ujumla ni nyenzo muhimu katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na tunapozungumzia uchumi wa viwanda hatuwezi kufanikiwa kama  hatutatoa kipaumbele katika teknolojia.”

“Lakini pia kama hatutakuwa makini katika kutumia tafiti  na uvumbuzi katika juhudi mbalimbali za maendeleo” amesema waziri huyo

Advertisement

Ametumia fursa hiyo kuwashukuru wafadhili wa kituo hicho Serikali ya Ujerumani ambao tayari wametoa kiasi cha Euro milioni  1.384  sawa na Sh3.5 bilioni kati ya  Euro  sawa na Sh4 milioni ambazo ni thamani ya mradi mzima utakaotekelezwa kwa miaka minne hadi 2021.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro akizungumza katika uzinduzi huo, ameishukuru Taasisi ya NM- AIST kwa kuendelea kushirikiana na wilaya hiyo katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kwa kuanzisha Kituo cha Umahiri cha TEHAMA.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza wa taasisi hiyo, Profesa Lughano Kusiluka amesema kituo hicho ni cha Jumuiya ya Afrika Mashariki ambacho kitakuwa kikifundisha wanafunzi katika ngazi za shahada ya umahiri katika teknolojia ya mambo ya simu hasa masuala ya  usalama wa matumizi ya simu na mawasiliano.

Amesema kwa sasa kimeanza na wanafunzi 27 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania imetoa wanafunzi 10 kati ya hao.

Meneja Mradi wa Kituo cha Umahiri cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka GiZ, Simon Hochstein amesema Serikali ya Ujerumani itaendelea kufadhili miradi mbalimbali katika elimu ya Juu na kuwataka wataalamu kuandaa maandiko ya miradi ili kupata fedha kama ilivyokuwa katika mradi wa Kituo hicho cha Umahiri.


Advertisement