Lissu azungumzia mshahara na kurejea kwake Tanzania

Thursday April 18 2019

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amedai kuwa uongozi wa Bunge la Tanzania umemlipa madai ya mishahara yake aliyokuwa akidai ya Januari hadi Machi 2019.

Amesema hayo leo Alhamisi Aprili 18,2019 kupitia ujumbe mfupi aliouweka katika mitandao ya kijamii akizungumzia afya yake na madai yake ya mishahara.

Lissu  aliyeko Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, 2017 mbali na mshahara wake pia amezungumzia afya yake akisema,“Na kwenye hili habari ni njema sana. Tarehe 2 ya mwezi huu nilikutana na madaktari wangu kwa appointment ya kwanza tangu operesheni za tarehe 20 Februari.”

“Taarifa yao ni kwamba mfupa wote wa mguu wa kulia umepona vizuri. Sehemu iliyowekewa 'kiraka' cha mfupa na kupigwa 'ribiti' ya chuma juu kidogo ya goti; na sehemu ya kwenye paja iliyotakiwa kuota mfupa mpya, zote ziko vizuri.”  

 “Sasa kazi kubwa iliyobaki ni kukunja goti na kujifunza kutembea tena. Naomba mniamini nikisema kujifunza kutembea tena, baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa kulala kitandani, ni kazi ngumu sana!!!!.”

Katika suala la kujifunza kutembea, Lissu amesema, “Nafikiri sina tofauti sana na mtoto mdogo anayejifunza kupiga hatua zake za kwanza. Lakini pole pole nitafika inshaallah.”

Advertisement

Amesema Mei 14, 2019 atapimwa urefu wa miguu ili atengenezewe kiatu au soli maalum kwa ajili ya mguu wa kulia.

“Kwa sababu ya majeraha makubwa niliyopata, mguu huo ni mfupi kwa sentimita kadhaa. Bila kiatu au soli maalum nitakuwa 'langara' na madaktari wamesema hiyo sio sawa sawa,” amesema.

Katika ujumbe wake huo, Lissu amesema, “Sasa nina tarehe ambayo madaktari wangu wamesema nitakuwa 'fiti' kurudi nyumbani.”

“Msiniambie niiseme kwa wakati huu. Tunahitaji kushauriana na wadau mbalimbali kuhusu tarehe halisi na namna bora zaidi ya kurudi kwangu nyumbani,” amesema

“Kwa hiyo, wakati muafaka utakapofika, hopefully (natumaini) sio mbali sana, nitawaeleza tarehe kamili ya kurudi nyumbani,” amesema.

Advertisement