VIDEO: Mabalozi wamlilia Mufuruki

Muktasari:

Kaimu balozi wa Marekani, Dk Inmi Patterson, balozi wa Ufaransa, Frederic Clavier na balozi wa Uingereza, Sarah Cook wameeleza jinsi mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki aliyefariki dunia juzi nchini Afrika Kusini alivyokuwa msaada kwa watu na nchi ya Tanzania.

Dar es Salaam. Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier na kaimu balozi wa Marekani, Dk Inmi Patterson wameeleza jinsi mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki alivyotumia uwezo wake kushirikiana na watu wengine.

Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cook amesema Mufuruki alikuwa rafiki mkubwa wa nchi yake na walifanya kazi kwa ushirikiano na kushauriana mambo mbalimbali.

Wametoa kauli hizo leo mchana Jumanne Desemba 10, 2019 katika shughuli ya kuaga mwili wa mfanyabiashara huyo katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

Mwili wa Mufuruki aliyefariki dunia juzi alfajiri uliwasili nchini jana jioni ukitokea Afrika Kusini, baada ya kuagwa leo utazikwa katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Balozi  Clavier amesema Mufuruki alikuwa mtu wa pekee aliyeweza kubadilisha utaalamu wake na wafanyabiashara,  wakuu wa nchi mbalimbali.

Amebainisha kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa mzalendo kwa bara la Afrika si Tanzania pekee.

"Katika maisha yangu nimekutana na watu wachache aina ya Mufuruki, alikuwa akiwasaidia vijana kukua kibiashara, mchango wake utaendelea kuishi ndani ya vijana wengi," amesema.

Clavier amesema mwaka 2019  Tanzania imewapoteza wafanyabiashara wakubwa wawili ambao ni Mufuruki na aliyekuwa mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi.

Katika maelezo yake balozi Saraha amesema Mufuruki alikuwa na mawazo ya kujenga na wakati mwingine alitoa changamoto kwa mambo ambayo hakubaliani nayo lakini kwa lengo la kujenga.

"Ali alikuwa rafiki wa ajabu alikuwa anakuja nyumbani tunaongea na kushauriana mambo mbalimbali. Tumepoteza rafiki ambaye tulifanya naye kazi kwa karibu, tulimuamini sana," amesema Balozi Cook

Dk Inmi  alieleza jinsi Tanzania ilivyopoteza mtu mwenye kujali maendeleo ya Watanzania na Taifa.

Amesema Mufuruki ni mfano wa kuigwa kwani licha ya familia yake kutokuwa na uwezo wa kumsomesha lakini alipambana mwenyewe hadi kufikia hatua aliyofikia.

“Mara ya mwisho kuonana alinipa kitabu cha maono ambacho kilibeba matumaini yote ya Watanzania na kinaonyesha jinsi alivyo mkarimu na mwenye moyo mwema. Mufuruki nitakukumbuka na Watanzania watakukumbuka pia,” amesema.

Kaimu mwenyekiti wa kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania,  Magreth Ikongo amesema Mufuruki alikuwa mtu wa kusikiliza nini mtu anasema.

"Wengi tunakosa sifa ya kusikiliza lakini yeye hata katika mikutano ya wanahisa alikuwa anaruhusu maswali na kuyajibu inavyostahili. Kwa niaba ya Vodacom tunashukuru tumepata bahati ya kuwa kiongozi wetu, alitoa miongozo mbalimbali katika kampuni hasa pale tulipopata changamoto mbalimbali,” amesema.