Magufuli: Hiki ni kipindi changu cha mwisho

Muktasari:

Rais John Magufuli ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020  na kubainisha kuwa baada ya kuibuka na ushindi ataliongoza Taifa la Tanzania kwa miaka mingine mitano  na ndio itakuwa ya mwisho.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020  na kubainisha kuwa baada ya kuibuka na ushindi ataliongoza Taifa la Tanzania kwa miaka mingine mitano  na ndio itakuwa ya mwisho.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumapili Novemba Mosi, 2020  jijini Dodoma baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi na mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage.

Amewashukuru Watanzania kwa ushindi huo na kusema ana deni kubwa la kuwalipa kwa imani kubwa waliyoionyesha kumchagua tena kuliongoza Taifa hilo kwa miaka mingine mitano.

“Ninaipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kufanikisha uchaguzi huu kwa kuwahisha matokeo. Ninawashukuru Watanzania kwa kunichagua tena…, hiki ni kipindi cha pili cha mwisho.”

 “Mmetupa ushindi mkubwa sana ambao umetuachia deni kubwa sana, ninamuomba Mungu anisaidie katika kipindi hiki cha pili tuweze kukidhi haja za Watanzania,” amesema Rais Magufuli ambaye ameshinda uchaguzi kwa kura 12,516,252.

Amesema ushindi huo siyo wake peke yake wala wa chama chake bali ni wa Watanzania wote. Amesema atawatumikia wote bila kujali wanapotoka, dini au kabila.

Amewapongeza baadhi ya wagombea wenzake kwa kukubali matokeo na kwenda kushiriki hafla hiyo akisisitiza kuwa ni ishara ya kukomaa kwao kisiasa.

 “Tutajitahidi kuzingatia maoni yenu hasa yale yenye lengo la kuiletea Tanzania maendeleo,” amesema kiongozi huyo.