VIDEO: Magufuli aahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi

Magufuli aahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi

Muktasari:

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli amesema baada ya uchumi wa Tanzania kuimarika sasa umefikia wakati wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Korogwe. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli amesema baada ya uchumi wa Tanzania kuimarika sasa umefikia wakati wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Ameeleza hayo leo Jumanne Oktoba 20, 2020 wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga katika mkutano wa kampeni, akisisitiza kuwa ili mipango mbalimbali iweze kufanikiwa ni lazima kujipanga kukusanya fedha na kutengeneza miundombinu.

“Maendeleo ni lazima yapangwe, bila kupangwa hakuna kitakachofanyika. Miaka mitano ilikuwa ya kujipanga ndio maana tulijenga  vituo vya afya, zahanati, hospitali za mikoa, rufaa lakini tukaongeza bima, bajeti ya madawa kutoka Sh31 bilioni hadi Sh270 bilioni, hayo yalikuwa maandalizi.”

“Uongozi ulio makini ni lazima upange maandalizi, bila hivyo itakuwa ahadi hewa. Ndio maana tulipoingia madarakani tu tuliongeza kukusanya fedha kutoka Sh850 bilioni hadi Sh1.5 trilioni, na hii ndio imetusaidia kujenga reli ya kisasa ambayo tunatumia Sh7.2 trilioni, pia tumeanza mradi wa umeme wa Julius Nyerere,” amesema Magufuli.

 

Ameongeza, “makusanyo na usimamizi makini ndio umetuwezesha kukarabati meli na kutoa elimu bure. Makusanyo ndio yamesaidia kufanya mabadiliko..., tukaanza kulipa malimbikizo ya wafanyakazi na tuko katika hatua za mwisho kulipa.”

“Sasa uchumi hujautengeneza unaanza kuzungumzia kupandisha mishahara. Ilikuwa ni kujenga uchumi kwanza ili uimarike.  Tulikuwa masikini sasa tupo katika  uchumi wa kati, tumefikia hapa kwa mipango mizuri iliyowekwa na serikali.”

Huku akishangiliwa na waliohudhuria mkutano huo amesema, “kwa sababu uchumi umeimarika na mapato yamekuwa mazuri, sasa katika kipindi cha miaka mitano tutaboresha maslahi ya wafanyakazi wa Tanzania.”