Majaliwa aipongeza Geita, atoa wito kwa mikoa mingine

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aridhishwa na matumizi fedha za kodi zinazotolewa na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) ataka mikoa mingine kuiga mfano wa jinsi Geita ilivyotekeleza miradi inayowanufaisha wananchi

Geita. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameupongeza mkoa wa Geita kwa usimamizi mzuri wa fedha za kodi zinazotolewa na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) ambazo zimetumika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Majaliwa amesema hayo leo Jumapili Septemba 22, 2019 mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa hospitali ya mkoa na kufungua nyumba za watumishi 10 ambazo zimejengwa kwa fedha kutoka serikali  pamoja na wawekezaji waliopo mkoani hapa.

Amesema mkoa wa Geita umeonyesha mfano mkubwa kwa fedha zinazolipwa na wawekezaji ambazo zimefanikisha ujenzi wa miradi ya afya, elimu, kujenga nyumba kwa ajili ya jeshi la polisi, magereza na kutaka mikoa mingine iige ili wananchi waone thamani ya uwekezaji.

Majaliwa amesema uratibu na matumizi mazuri wa fedha za kodi ya huduma zinazotolewa na GGM lazima zirudi kwa wananchi ili waweze kujenga imani na uwekezaji uliopo kwenye maeneo yao.

Amesema ili huduma za afya ziwafikie wananchi ni lazima miundombinu iimarishwe na kuzitaka halmashauri kusimamia ujenzi wa zahanati kila kijiji.

Amesema serikali imeamua kujenga vituo vya afya kila kata ambapo kwa mwaka 2018 vituo 352 vimejengwa na ujenzi wa hospitali 69 na hospitali za mikoa mipya saba ikiwemo Geita ujenzi unaendelea.

Aidha amepongeza juhudi zinazofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kujenga na kukamilisha miradi kwa wakati tofauti na ilivyokuwa awali.

Akizungumzia nyumba za watumishi, Majaliwa ametaka watumishi kujali na kutunza nyumba hizo na kukemea tabia ya watumishi kukaa kwenye nyumba za serikali na kuziacha mbovu na kutaka mkoa uendelee kujenga nyumba nyingi zaidi kwa watumishi.

Awali, Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Geita, Deodatus Kayango amesema nyumba 10 zilizojengwa kwa ajili ya wakuu wa idara kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa zimegharimu Sh992 milioni na itakabilima Novemba 2019.

Naye meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoani Geita, Glad Jefta amesema hospitali hiyo itakayokuwa na majengo 16 inatarajiwa kugharimu Sh5.9 bilioni.

Amesema hospitali hiyo itakuwa na vitanda 486 na itakua na uwezo wa kutoa huduma kwa wa gonjwa 1,000 kwa siku.