Makonda ataka mahubiri kufanyika klabu za usiku Dar

Sunday September 08 2019
makonda pic

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema atatoa kibali kwa viongozi wa dini kwenda kuhubiri neno la Mungu usiku katika klabu mbalimbali za muziki.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumapili Septemba 8, 2019 katika Kanisa la Inuka Uangaze la Mtume  Boniface Mwamposa  maarufu 'Bulldozer' lililopo Kawe, Dar es Salaam.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema amekuwa akitembea kwenye klabu hizo za usiku na kuwaona watu wakicheza kwa furaha lakini hawaonekani kufahamu kuhusu uwepo wa Mungu.

“Watumishi wa Mungu kama mnataka kuhubiri kwenye klabu nawapa kibali mkawahubirie huko angalau kwa nusu saa wapate fursa ya kusikia neno la Mungu, wasije kusema hawakusikia. Wafuateni huko.”

“Mtumishi wa Mungu yeyote akitaka kwenda klabu ruksa. Sasa nimuone huyo mwenye klabu akatae mimi si ndio mkuu wa mkoa. Kuanzia wiki ijayo mkitaka kwenda klabu yoyote mniambie kapigeni kwa nusu saa,” amesema Makonda.

Advertisement