Makonda awanyoshea kidole Halima Mdee, Kubenea na Mnyika

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amedai  wabunge watatu wa upinzani wa majimbo ya Dar es Salaam hawawatumikii wananchi kwa sababu hawafiki kwenye shughuli za maendeleo kuelezea shida za majimbo yao.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amedai  wabunge watatu wa upinzani wa majimbo ya Dar es Salaam hawawatumikii wananchi kwa sababu hawafiki kwenye shughuli za maendeleo kuelezea shida za majimbo yao.

Wabunge hao wa Chadema ni Halima Mdee (Kawe), Saed Kubenea (Ubungo) na John Mnyika (Kibamba).

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 26, 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) muda mfupi kabla ya kuwasili kwa ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania.

Katika hafla ya mapokezi ya ndege hiyo iliyohudhuriwa na Rais John Magufuli, mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema, “bahati  mbaya tuna majimbo matatu tulikosea wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam jimbo la Kibamba, Ubungo na Kawe. Wabunge wake si tu kwamba sio watumishi wa wananchi  lakini pia ni wezi wanaokula posho bungeni bila ya kufanya kazi kwa wananchi.”

“Wilaya ya Ubungo ina wabunge wawili na meya wa upinzani (Boniface Jacob). Hawawezi kuja kwenye shughuli yoyote ya maendeleo,  wangeweza kufika hata kwenye shughuli ya leo wakawa sauti ya wananchi lakini hawawezi,” amesema Makonda.

Ameongeza, “lakini  kwa sababu umeniteua kuwa mkuu wa Mkoa naomba nipaze sauti na kutoa kilio cha wananchi wa Ubungo ikipendeza Rais usikie kilio chao.”

Makonda amesema Ubungo hakuna Hospitali ya Wilaya na wananchi wake wanalazimika kusaka huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni.

“Wabunge wao hawajawahi kutoa hata shilingi, hawajawahi kumbana waziri, kujenga hoja kwenye manispaa ili wawe na bajeti ya kujenga hospitali ya wilaya. Wananchi wa Ubungo afya zao zipo matatani wabunge wao wameingia mitini.

Naomba unisaidie Sh1.5 bilioni niwajengee hospitali ya wilaya,” amesema Makonda.