Mamia ya waombolezaji washiriki ibada mazishi ya Mwanakotide

Matilda Charles ambaye ni mke wa marehemu, Fulgency Mapunda maarufu ‘Mwanakotide’ akitoa heshima za mwisho kwa mume wake wakati wa misa ya kumuaga iliyofanyika katika kanisa la katoliki parokia ya moyo mtakatifu wa yesu lililopo Manzese jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Mamia ya waombolezaji leo Jumatano Oktoba 9, 2019 wamejitokeza katika Kanisa Katoliki Manzese jijini Dar es Salaam kushiriki ibada ya mazishi ya aliyekuwa kada wa Chadema, Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotide.

Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji leo Jumatano Oktoba 9, 2019 wamejitokeza katika Kanisa Katoliki Manzese jijini Dar es Salaam kushiriki ibada ya mazishi ya aliyekuwa kada wa Chadema, Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotide.

Mwanakotide alifariki dunia Jumapili Oktoba 6, 2019 katika Hospitali ya St Monica, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa.

Alikuwa mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za hamasa za chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kujizolea umaarufu kupitia mikutano ya hadhara ya chama hicho, zikiwemo kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na 2015.

Viongozi wa Chadema katika ibada hiyo wanaongozwa na katibu mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Dk Vicent Mashinji.

Viongozi wengine wa chama hicho waliohudhuria ibada hiyo ni manaibu katibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) na mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea.

Katika ibada hiyo salamu za makundi mbalimbali zitatolewa na waombolezaji hao kuaga mwili wa Mwanakotide kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Ruvuma kwa mazishi.