Maombi ya Tundu Lissu kupinga kuvulia ubunge haya hapa

Monday September 2 2019

Tundu Lissu, mwananchi habari, kesi tundu lissu,Mahakama Kuu ya Tanzania ,Maombi ya Tundu Lissu kupinga kuvulia ubunge

Mawakili wa Serikali na Mwakili upande wa  Tundu Lissu wakiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo kusikiliza uamuzi. Picha na Anthony Siame 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Hatimaye Mahakama Kuu ya Tanzania leo Jumatatu Septemba 2, 2019 imesikiliza maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ya kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika wa Bunge ya kukoma kwa ubunge wake huku akieleza sababu za kuomba kibali hicho.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Lissu kupitia kwa jopo la mawakili wake linaloongozwa na Peter Kibatala pamoja na mambo mengine amedai hatua ya Spika kutoa taarifa kuwa ubunge wake umekoma haikuzingatia matakwa ya kisheria.

Kibatala ameeleza hakupewa haki ya kusikilizwa kabla ya uamuzi huo na kwamba wala hakuwahi kuelezwa sababu za kukoma kwa ubunge wake, huku akidai Spika ambaye ndio alikuwa mlalamikaji na jaji katika kesi yake hiyo.

Wakili Kibatala ambaye katika hoja zake amewasilisha mahakamani kesi mbalimbali zilizokwishakuamuriwa na Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na hata mahakama za nje, amesema jambo ambalo ni kinyume cha misingi ya haki ya asili ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa.

Amesema kwa mujibu wa maombi katika viapo vyao kinzani, wanatoa tafsiri ya kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kumtaarifu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa kiti cha jimbo la Singida Mashariki kiko wazi si tamko la kumvua ubunge.

Hata hivyo, amesema jukumu la kutafsiri sheria ni la Mahakama na si la mtu mwingine yeyote.

Advertisement

Katika hatua nyingine, Wakili Kibatala ameiomba Mahakama hiyo itoe amri za kusitisha kwa muda kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo Miraji Mtaturu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kusubiri kumalizika kwa mashauri hayo.

Wakili Kibatala ameieleza mahakama kuwa vikao vya Bunge vinatarajia kuanza kesho Jumanne na kwamba kwa mujibu wa taratibu za bunge moja ya shughuli zitakazofanyika kabla ya shughuli nyingine za kawaida za Bunge ni kuapishwa kwa Mtaturu.

“Kama Mtaturu akiapishwa, Mheshimiwa Jaji kazi ya Mahakama hii itakuwa ngumu na hata kwa mwombaji itakuwa vigumu kulinda haki zake. Na hata mwenendo huu hautakuwa na maana,” amesema wakili Kibatala

“Kwa misingi hii Mahakama inaweza kutoa amri kuhusu ombi si (kusimamisha kwa muda kuapishwa kwa Mtaturu), hata kabla ya kutoa uamuzi wa ombi la kibali.”

Pamoja na mambo mengine pia Kibatala ameelezea mazingira ya Lissu kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge pamoja na kutoa tamko la mali na madeni yake katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma akisema ni kwa sababu ya ugonjwa.

Katika hilo, Wakili Kibatala pia ameelezea tukio zima la kushambuliwa kwa Lissu akirejea maelezo ya Lissu mwenyewe katika maelezo yake ya maandishi pamoja na hati za viapo vinavyounga mkono maombi hayo.

Baada ya mawakili wa Lissu kumaliza kuwasilisha hoja zao, kwa sasa mawakili wa Serikali wanajibu hoja za mawakili hao wa Lissu, kabla ya mawakili wa  Lissu kusimama tena kujibu hoja zilizoibuliwa na mawakili wa Serikali.

Lissu amefungua maombi Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kumwakilisha, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa ubunge wake na mahakama iteunge taarifa hiyo.

Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.


Advertisement