Matiko aomba ushirikiano kuimarisha Chadema, Heche akubali kushindwa

Muktasari:

Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu imefanya uchaguzi wa viongozi wake watakaokiongoza kwa miaka mitano ijayo.

Shinyanga. Mwenyekiti mpya wa Chadema Kanda ya Serengeti, Esther Matiko amewaomba viongozi wa sasa, waliopita pamoja na wanachama wa chama hicho kushirikiana kukijenga na kukiimarisha chama ili kushinda chaguzi zijazo.

Akishukuru baada ya kuchaguliwa kwa kura 44 dhidi ya mshindani wake John Heche aliyepata kura 38 jana Jumapili Desemba 1, 2019, Matiko ambaye pia ni mbunge wa Tarime mjini alisema kura alizopata zinaonyesha imani kwake na kuahidi kufanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuijenga Chadema katika kanda hiyo.

Heche ambaye pia ni mbunge wa Tarime vijijini ndiye alikuwa mwenyekiti wa kanda hiyo tangu mwaka 2014.

Matiko aliwaambia wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi uliosimamiwa na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kuwa umoja na ushirikiano miongoni mwa viongozi, wanachama na wananchi ndiyo siri ya mafanikio na kuwaomba wagombea wote kuvunja makambi kwa sababu baada ya uchaguzi kambi inayosalia ni ya Chadema.

Baada ya matokeo hayo, Heche alitumia ukurasa wake wa Twitter kuzungumza uchaguzi huo akisema, “nawashukuru sana wanachama wenzangu na wajumbe kwa kura mlizonipa japo hazikutosha.”

“Nawapongeza wote waliotumia demokrasia yao kuchagua wagombea wenzangu. Nawatakia kila la heri walioshinda katika majukumu magumu mbele yetu. Hakuna kulala," aliongeza

Nafasi ya Makamu mwenyekiti ilinyakuliwa na Gimbi Masaba kwa kupata kura 45 dhidi ya washindani wake King Tarai aliyepata kura 28 na Jackson Luyombya alinyakua kura 12.

Maendeleo Makoye alichaguliwa kwa kura 43 kuwa mweka hazina wa kanda hiyo akimbwaga mbunge wa viti maalum, Catherine Ruge aliyepata kura 32.

Mkutano huo wa uchaguzi ulihudhuriwa na wajumbe 85. Kanda ya Serengeti katika mfumo wa uongozi wa Chadema inaundwa na mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga.