MITAZAMO TOFAUTI: Mbowe, wasomi wachambua tahadhari ya CCM kuanguka

Mwanza. Onyo alilotoa Rais John Magufuli, ambaye ni mwenyekiti wa CCM, kwa viongozi wa chama hicho tawala kuwa wasipoangalia kinaweza kuanguka, linaweza kuwa tahadhari mahsusi wakati huu, lakini baadhi ya wasomi na wanasiasa wana mawazo tofauti.

Rais Magufuli alisema hayo wakati akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM jijini Mwanza Alhamisi iliyopita, akisema CCM inaweza kupoteza dola iwapo viongozi wake watajisahau na kuongoza kwa mazoea bila kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi.

Sehemu hiyo ya hotuba yake mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM--chombo cha pili kwa mamlaka baada ya Mkutano Mkuu imeibua mijadala, wengi wakihoji sababu za kutoa kauli hiyo wakati huu.

Wako wanaoona kuwa Rais ameona mbali baada ya kukiongoza chama hicho kwa miaka minne, wapo wanaoona ni tahadhari ya kawaida na wapo wanaoona nguvu ya upinzani ikiongezeka.

Rais ametoa tahadhari hiyo katika kipindi ambacho vyama vya siasa vinajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2020 baada ya uliopita kuwa na ushindani mkali kuliko wakati mwingine wowote tangu kurejeshwa kwa vyama vingi mwaka 1992.

Katika uchaguzi huo, Magufuli alishinda kwa kupata kura milioni 8.8, sawa na asilimia 58, kiwango ambacho ni kidogo tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995.

Pia katika uchaguzi huo, vyama vya upinzani viliingiza wabunge wengi takriban theluthi moja ya wabunge wote tofauti na miaka mingine, kushika serikali kadhaa za mitaa na kupata idadi kubwa ya madiwani.

Baadhi ya viongozi hao waliamua kutangaza kujivua nafasi zao kwa kile walichosema “kuunga mkono juhudi za Rais”.

Ukiacha vyama vya ukombozi vilivyoanguka kusini mwa Afrika, Rais ametoa tahadhari hiyo katika muda ambao vyama tawala vinaendelea kuanguka, ama katika sanduku la kura ama kwa nguvu za wananchi kama ilivyokuwa nchini Sudan, Algeria, Ghana, Sierra Leona na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Rais pia ametoa tahadhari hiyo wakati akiwa mmoja wa viongozi wa juu wa Serikali ambaye amekuwa akikumbana na mabango yanayozungumzia shida za wananchi ambazo hazikuweza kutatuliwa na viongozi wa eneo husika na hivyo kumlazimisha kuwawajibisha wahusika kwa kutaka wachukue hatua au kuwatumbua.

Lakini pia ametoa tahadhari hiyo ikiwa ni ndani ya mwezi mmoja baada ya CCM kupata ushindi wa asilimia 99 katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, matokeo ambayo yangeweza kumaanisha kuwa upinzani unaelekea kuisha.

Tahadhari hiyo pia imetolewa katika kipindi ambacho wengi wanaona kama siasa za upinzani zimedhoofishwa na amri ya kuzuia maandamano, mikutano ya hadhara na kwa kiasi fulani mikutano ya ndani kuzuiwa na Jeshi la Polisi.

Lakini mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anasema hatua hizo hazijadhoofisha upinzani, bali kuuimarisha.

“Unapozuia chaguo la wananchi la chama mbadala, uhuru wa watu, uhuru wa kujieleza ni hatari,” anasema mbunge huyo wa Jimbo la Hai.

“Na kuua upinzani ni ngumu kwa kuwa upinzani si Chadema. Upinzani upo katika maisha ya watu na watu ndiyo wanahitaji chama mbadala.

“Kwa miaka minne, Serikali ya Awamu ya Tano ilijitahidi kuizima ndoto hii ya jamii ya kuwa na chama mbadala, lakini walisahau ndoto ya jamii haipigani kwa silaha au nini, inapigana kwa hisia, fikra na matamanio ya watu.”

Mbowe ni mmoja kati ya watu waliohojiwa na Mwananchi kuhusu maana ya tahadhari ya Rais katika kipindi hiki.

“Anachokiongea Magufuli sasa na kukipigania hakipo. CCM imebaki chama dola ambacho kinapumulia mashine,” alisema Mbowe.

“CCM imepoteza mvuto na hilo lilijidhihirisha katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2015. Tuwaache wafu wazike wafu wenzao kwani kama yeye analiona hilo leo, sisi tumeliona zamani na tunasonga mbele. Kama Rais amekuja kulitambua dakika hii, basi Mungu anamsaidia kutambua hilo ambalo sisi tumeliona zamani.

“CCM kwa sasa haiwezi kujenga ushawishi tena, imebaki historia. Yeye na chama chake walikusudia kuua upinzani lakini imeshindikana.”

Mbowe alisema uhai wa vyama vya siasa kwa kiasi kikubwa ni hitaji la jamii.

Chadema, chama kikuu cha upinzani nchini, iliingiza wabunge 70 mwaka 2015 kutoka 48 wa mwaka 2010, ilipoteza wabunge saba waliohamia CCM kwa maelezo ya “kuunga mkono juhudi za Rais”.

Lakini mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema alikuwa na mtazamo tofauti kuhusu nguvu ya CCM.

“Nadhani tahadhari hii imekuja wakati mwafaka kwa sababu ikijisahau na kubaki kujisifia kuwa chama cha ukombozi, itang’olewa madarakani.

“Mwalimu (Julius) Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu kwenda kuiimarisha na kuifanya Tanu kuwa chama cha watu; misingi hii ndiyo inayoifanya CCM kuendelea kuwa imara.”

Profesa Mpangala alisema watu wanaiona CCM imebadilika kutokana na kuacha misingi ya Azimio la Arusha lililohimiza haki na usawa kwa wote, umoja na mshikamano.

Ushindi wa bila kupingwa

Profesa Mpangala pia aliangalia uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ulioipa CCM ushindi wa asilimia 99 kuwa ni moja ya mambo ambayo Mwalimu Nyerere asingeyakubali.

“Mbinu zinazotumika sasa kuipa ushindi CCM na wagombea wake si sahihi. Vyama vyote vya siasa vipewe haki sawa ya kufanya siasa kunadi sera na kutafuta uungwaji mkono kwa mujibu wa sheria,” alisema na kuongeza Profesa Mpangala.

“Chaguzi zetu zitoe haki na fursa kwa wananchi kuwachagua viongozi wanaowataka kuanzia ngazi ya vijiji na mitaa badala ya kupandikiziwa kwa madai ya kupita bila kupingwa kama tulivyoshuhudia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.”

Lakini mtaalamu wa masuala ya afya ya jamii, Dk Albert Komba anaona tahadhari hiyo ya Rais imezingatia viongozi kutoguswa na mambo yanayoendelea katika jamii inayobadilikabadilika kulingana na hali.

“Uongozi wa taasisi yoyote ni suala la watu na nini kinafanyika kwa ajili ya watu. Kila kinachofanyika lazima kifanyike kwa ajili ya mahitaji na maslahi ya watu. Nadhani ndiyo tahadhari anayotoa Rais Magufuli,” alisema.

Dk Komba alisema viongozi wa taasisi zote zinazohudumia wananchi, na hasa vyama vya siasa, lazima wasikie, kuangalia, kuhisi na kujua jamii inataka nini kulingana na wakati, mahitaji na maendeleo.

“CCM lazima ijipime kwa uimara na ufanisi wake kupitia huduma za kijamii, maisha bora, huru na maendeleo kulingana na muda na mahitaji ya watu. Viongozi lazima watambue kuwa hawapo wala hawaongozi kwa ajili yao; bali Watanzania zaidi ya 55 milioni,” alisema Dk Komba.

Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa alisema Rais Magufuli asiishie kuihadharisha CCM pekee, bali aende mbali kwa kutumia nafasi yake kukuza, kulinda na kuendeleza demokrasia nchini.