Mbowe alazwa Aga Khan

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe anaumwa na amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam tangu  Novemba 17, 2019.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe anaumwa na amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam tangu  Novemba 17, 2019.

Mbowe ni miongoni mwa viongozi tisa wa Chadema wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi namba 112/ 2018 inayoendelea leo Jumanne Novemba 19, 2019 kwa hatua ya utetezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Alitakiwa kuendelea kujitetea leo lakini mdhamini wake,  Greyson Selestine ameieleza mahakama hiyo kuwa mbunge huyo wa Hai anaumwa na amelazwa katika hospitali hiyo.

“Mbowe amelazwa tangu Novemba 17 katika hospitali ya Aga Khan,” amesema Selestine bila kueleza mwenyekiti huyo wa Chadema anaumwa nini.

Kinachoendelea katika kesi hiyo ni washtakiwa wanne, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Ester Bulaya (Bunda), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Halima Mdee (Kawe) kujitetea kwanini wasifutiwe dhamana.

Ijumaa iliyopita Novemba 15, 2019, mahakama hiyo ilitoa amri ya kukamatwa kwa washtakiwa hao kutokana na kukiuka masharti ya dhamana baada ya kutofika  mahakama kusikiliza kesi hiyo.

Siku hiyo wenzao watano ambao ni Mbowe, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji; naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) na Esther Matiko (Tarime Mjini) walifika mahakamani hapo.

Amri ya kukamatwa kwa wabunge hao wanne ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya washtakiwa hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote wala wadhamini wao.

Kuwa shakani kwa dhamana ya wabunge  hao kumekuja ikiwa imepita miezi nane tangu Mbowe na Matiko kuachiwa huru kutoka mahabusu baada ya kufutiwa dhamana na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Walifutiwa dhamana hiyo Novemba 23, 2018.

Katika kesi hiyo wote kwa pamoja wanakabiliwa na  mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea mahakamani kuhusu dhamana ya wabunge hao na afya ya Mbowe