Mchungaji Msigwa azungumzia migogoro ilivyomalizwa Chadema

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, aliyemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa akizngumza kwenye mkutano mkuu wa Chadema kanda hiyo jijini Mbeya ambao unafanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa kanda hiyo. Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amesema katika kanda hiyo iliibuka migogoro iliyotishia uhai wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania 

Mbeya. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amesema katika kanda hiyo iliibuka migogoro iliyotishia uhai wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Mchungaji Msigwa ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini ametoa kauli hiyo leo Desemba Mosi, 2019 katika mkutano mkuu wa chama hicho kuchagua viongozi  wa kanda ya Nyasa unaofanyika mjini Mbeya. Mchungaji Msigwa anagombea uenyekiti wa kanda hiyo.

Amesema katika mikoa mitano ya Kanda hiyo kulikuwa na migogoro iliyotokana na matokeo ya chaguzi mbalimbali ndani ya chama hicho na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Tulipoingia kwenye uongozi wa kanda hii changamoto tuliyokumbana nayo ikatutesa ni migogoro, kulikuwa na mgogoro Iringa, Njombe, Mbarali, Kyela, Rukwa, Sumbawanga. Kulikuwa na migogoro kila mahali kwenye chama hiki,” amesema Mchungaji Msigwa.

Amesema walihakikisha wanaifanyia kazi na sasa hali ni shwari.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Chadema Kanda hiyo, Emmanuel Masonga amesema viongozi wakubwa ndani ya chama hicho ndio walikuwa chanzo kutokana na maslahi yao.

“Ni kweli kulikuwa na migogoro mikubwa, ukienda  Rukwa kulikuwa na mgogoro kati ya Sadrick Malila na Aida Kenani, hata kule Njombe mimi mwenyewe nilikuwa sehemu ya migogoro. Ninashukuru  tumelishughulikia na kumaliza kwa kiasi kikubwa,” amesema Masonga.

Amesema kupitia mchakato wa Chadema ni msingi kuanzia ngazi ya chini ulisaidia kumaliza migogoro katika chama hicho.