Meya Jacob asema fedha alizoomba Makonda ujenzi hospitali Ubungo zilishapitishwa siku nyingi

Saturday October 26 2019
meyapic

Dar es Salaam. Meya wa Ubungo, Boniface Jacob amesema Sh1.5 bilioni ambazo mkuu wa Mkoa wa Dar es Slaam, Paul Makonda amemuomba Rais John Magufuli kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Ubungo zimeshatolewa siku nyingi na Serikali.

Jacob ametoa maelezo hayo leo jioni Jumamosi Oktoba 26, 2019  saa chache baada ya Makonda kumuomba Rais Magufuli kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali kwa maelezo kuwa wakazi wa wilaya hiyo wanalazimika kwenda wilaya ya Kinondoni kusaka huduma za afya.

Makonda alitoa kauli hiyo katika hafla ya kupokea ndege mpya ya pili ya Boeing 787-800 Dreamliner iliyowasili leo saa 8:36 mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ikitokea nchini Marekani.

Katika maelezo yake Jacob amesema, “Rais Magufuli leo nimekusikia ukimjibu Makonda kuwa unatupatia watu wa Ubungo Sh1.5 bilioni  za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya baada ya Makonda kukuomba.”

“Rais nakukumbusha wewe na wasaidizi wako wote kuwa Februari 28, 2019 baraza la manispaa Ubungo lilipitisha Sh84 bilioni kuwa bajeti yake ya 2019/2020. Katika bajeti hiyo manispaa tulitenga Sh250 milioni kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, na tukaiomba Serikali kupitia ruzuku za miradi ya maendeleo mnazotushushia mtuletee Sh1.5 bilioni.”

Jacob amesema Julai 2019 Bunge lilipitisha bajeti ya Wizara ya Tamisemi, yakiwemo maombi ya fedha zote, “ile ya Wilaya na zile za mapato ya Halmashauri. Julai hiyo wakati tunafunga mkutano mwisho wa mwaka  2018/2019 katika baraza la madiwani nikakushukuru (Magufuli)  na Serikali kuu kutushushia Sh3 bilioni.”

Advertisement

“Fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya halmashauri, kwamba Sh1 bilioni ya ujenzi wa kituo cha afya Kimara Mwisho  na hizo Sh1.5 bilioni za  ujenzi wa Hospitali ya wilaya.”

Jacob amesema Makonda ameomba fedha ambazo tayari Rais Magufuli alikuwa ameshazifanyia kazi.

“Leo si unaona (Makonda) kakuomba tena kitu kilekile ulichokuwa tayari umeshakifanyia kazi na kukipatia ufumbuzi,” amesema Jacob.


Advertisement