Mfanyabiashara Yusufali afutiwe kesi, akamatwa tena

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia mashtaka mfanyabiashara maarufu,  Mohamed Yusufali na mwenzake Arital Maliwala


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia mashtaka mfanyabiashara maarufu,  Mohamed Yusufali na mwenzake Arital Maliwala.

Hata hivyo, washtakiwa hao baada ya kufutiwa kesi hiyo na kutoka katika chumba cha mahakama, walikamatwa na kupelekwa mahabusu.

Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka yao leo Februari 5, 2019  mbele ya Hakimu,  Janeth Mtega baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.

Yusufali na mwenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 601 ikiwamo kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh14.9 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 4/2019.

Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai amedai mbele ya hakimu Mtega kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.

Swai , amedai  kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.

Hakimu Mtega amesema kutokana na maombi hayo, mahakama imeifuta kesi hiyo.

Hii ni mara pili, kwa Yusufali kufutiwa kesi katika mahakama hiyo kwani  Januari 11, 2019,  DPP alimfutia mashtaka baada kueleza kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.