Misitu ya Amazon Brazil yaungua mara 73,000

Muktasari:

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro ameshutumu mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuhusika na matuki hayo.

Salvador, Brazil. Matukio ya moto 73,000 yemeripotiwa kutokea katika Misitu ya Amazon iliyopo Kaskazini mwa Brazil katika kipindi cha miezi minane.

Inaelezwa kuwa idadi hiyo iliyorekodiwa kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu ni kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 2013.

Kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Nafasi (INPE), matukio ya moto katika misitu hiyo yameongezeka kutoka 39,759 kwa mwaka 2018 mpaka 73,000.

Taarifa ya INPE ambayo ndiyo wakala uliopewa jukumu la kusimamia kuhifadhi misitu hiyo inasema matukio hayo yameongezeka kutokana na ukataji miti ovyo.

“Matukio ya moto katika misitu hiyo huongezeka wakati wa msimu wa kiangazi na kumalizika mwishoni mwa Oktoba au Novemba mwanzoni,” inasema taarifa hiyo ya INPE.

Shirika la Kimatifa la Mazingira Duniani (WWF), limelaani ongezeko la matukio ya moto katika misitu hiyo na kutahadharisha kuwa yataathiri mabadiliko ya hali ya hewa.

Hata hivyo, Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro ameyashutumu mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuhusika na matukio hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Bolsonaro alisema, “hatua ya taasisi hizo kutoa tahadhari dhidi yangu na Serikali ya Brazil inaweza kuwa sababu ya moto katika msitu huo.”