MPYA: Mjane wa bilionea aliyeuawa Kenya anyimwa urithi

Muktasari:

Sarah Wairimu kupitia kwa wakili wake amekataa kuutambua wosia huo na kudai kuwa ni batili kwa kuwa ana haki ya kumiliki mali za mumewe.

Nairobi, Kenya. Wosia wa bilionea aliyeuawa Kenya, Tob Cohen haujamtaja mjane wake.

Sara Wairimu ambaye alikuwa mke wa ndoa wa mfanyabiashara huyo amenyimwa urithi wa mali zote za mume wake ambaye kabla ya kifo chake walikuwa na kesi ya talaka.

Bilionea Cohen aliuawa na kisha mwili wake kupatikana katika tanki la maji nyumbani kwake.

Jeshi la Polisi nchini humo linamshikilia mwanamke huyo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mfanyabishara huyo kwa kushirikiana na watuhumiwa wengine.

Kwa mujibu wa wosia huo uliosomwa Ijumaa iliyopita, asilimia 50 ya nyumba yake amemuachia dadake, Gabrielle Van, 25 amewapa wapwa zake (watoto wa dada yake huyo) na  25 iliyobaki amempa ndugu yake mwingine aitwaye Bernard.

Wosia huo pia ulisema kuwa fedha zote zilizopo katika akaunti za benki apewe dada yake Gabrielle.

Hata hivyo, wosia huo haukumtaja mjane wa mfanyabisahara huyo na kutompa chochote.

Kufuatia hali hiyo wakili wa mjane huyo, Philip Murgor amepinga wosia huo na kusema kuwa Sarah ana haki ya kurithi mali za mumewe.

Wakili Murgor alisema kuwa watahakikisha wanafuata sheria kupinga wosia huo ili mteja wake apate haki yake.

Ijumaa iliyopita wosia huo ulioachwa na bilionea Cohen uliwekwa hadharani mbele ya familia yake.

Wosia huo ulifunguliwa mbele ya wanafamilia na marafiki wa bilionea huyo jijini Nairobi.

Hata hivyo, mke wa mfanyabishara huyo, Sarah Wairimu ambaye kwa sasa anashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mumuwe kupitia wakili wake alikataa kuutambua wosia huo na kusema kuwa ni batili.

Aprili mwaka huu Sarah na Cohen walifungua kesi ya talaka ambayo haikuamuriwa mpaka mfanyabishara huyo alipopoteza maisha.

Awali wakili wa mfanyabishara huyo, Chege Kirundi, ambaye ndiyo msimamizi wa wosia huo aliwaambia waandishi wa habari kwamba yaliyomo katika wosia huo yatabaki kuwa ya binafsi isipokuwa kama familia ya Cohen itaagiza vingine.

“Hatutajadili maelezo yoyote yaliyomo kwenye wosia huo kwa wakati huu,” alisisitiza wakili Kirundi na kuongeza kuwa wosia huo utasomwa wakati suala hili litakapofika mahakamani kwa ajili ya kusikilizajwa

Kwa upande wake wakili Cliff Ombeta, anayemwakilisha dada wa bilionea huyo, Gabrielle Van Straten alisema mawakili wa Sarah walialikwa kwenye hafla hiyo lakini walikataa kwa maelekezo kutoka kwa mteja wao.

“Tulimwalika Sarah lakini hajafika. Tumewasubiri kwa muda mrefu lakini hawajafika wala hawakutuma mwakilishi,” alisisitiza wakili huyo.

Hata hivyo, familia ya mfanyabishara huyo akiwamo kaka yake Bernard waligoma kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa zaidi za wosia huo. kama umemtenga mwanamama huyo.

Marehemu Cohen imeacha kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti za benki, hisa katika kampuni mbalimbali na mali isiyohamishika.

Wakili wa Sarah azungumza

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, wakili Murgor alisema wakili wa marehemu Cohen na familia yake wametenda vibaya.

“Kufungua wosia wa marehemu wakati mjane yuko kizuizini ni kitendo kisichokubalika na kina leta hisia tofauti wakati tayari kulikuwa na uvujaji wa yale yaliyomo,” alisema Murgor.

Wakili huyo alisema Sarah anatarajia kupigania jaribio lolote la kutakatisha mali ambayo ni halali kwake.

“Nilikuwa na yeye (Sarah) jana ninachoweza kusema ni kwamba ikiwa kuna jaribio la kuingilia haki zake za mali katika nyumba yake au hata katika kampuni, atahakikisha anapigania haki hiyo mahakamani.

“Mtu yeyote akiwa na madai juu ya nyumba hiyo iliyopo eneo la Kitisuru au mali zake anapaswa kwenda mahakamani na si vinginevyo  kwa sababu ndoa ya Sarah na Cohen haikuwahi kuvunjika.