Msechu awapagawisha washiriki Jamafest

Msanii Peter  Msechu akiimba wakati wa ufunguzi wa Tamasha Jamafest-2019 linalofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam leo

Muktasari:

Miondoko ya zamani na sasa aliyotumbuiza msanii wa kizazi kipya nchini Tanzania, Peter Msechu kwenye Tamasha la Utamaduni la Afrika Mashariki  (Jamafest) linaloendelea jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imewasahaulisha kwa muda washiriki kuangalia ngoma za nchi mwao na kujumuika pamoja kucheza.

 

Dar es Salaam. Mwanamuziki kutoka Tanzania, Peter Masechu amepagawisha washiriki wa Tamasha la Utamaduni la Afrika Mashariki  (Jamafest) kwa kuimba nyimbo za dansi za zamani ikiwamo wimbo maarufu 'Rangi ya Chungwa'.

Msechu alipagawisha washiriki kutoka washiriki wa Tamasha hilo kwa kuimba wimbo wa 'Neema' wa DDC Mlimani Park Sikinde ukafuata  Rangi ya Chungwa ulioimbwa na Nyanyembe Jazz na kuweka vionjo vya bendi ya Fm Academia  'Utamu wa Vannila'.

Katika kuonyesha wamevutiwa na nyimbo hizo kutoka nchini Tanzania washiriki kutoka nchi za Burundi na Rwanda walisogea mbele ya jukwaa na kuanza kucheza.

Msechu akitumbuiza leo Jumapili Septemba 22, 2019 katika siku ya pili kati ya tamasha hilo linaloendelea kwenye Uwanja wa Taifa na Uhuru, Dar es Salaam.

Msanii huyo alitumia kipaji chake kwa kuchanganya miondoko ikiwamo ya singeli kwa kuimba wimbo wa Afrika Mashariki katika mahadhi hayo huku akinakshi kwa kuzitaja nchi washiriki wa shindano hilo amabzo ni Kenya,Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani ya Kusini na mwenyeji Tanzania.