Mtume Mwingira amtaka Mbowe kuwa mvumilivu

Saturday February 22 2020

 

By Fortune Francis na Sanjito Msafiri, Mwananchi [email protected]

Kibaha. Mtume na Nabii wa Kanisa la Efatha nchini Tanzania, Josephat Mwingira

amemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini humo, Freeman Mbowe kuwa mvumilivu ili ale mbivu.

Mtume Mwingira ameyasema hayo leo Februari 22,2020 wakati akitoa shukrani katika msiba wa baba yake Elias Mwingira aliyefariki dunia Februari 22, 2020.

Amesema nchi inahitaji watu wavumilivu watakaoongoza nchi na sio wahuni.

"Mbowe wewe umebanwa na umeminywa sana, nimegundua jambo kwako wewe ni mvumilivu sana na mvumilivu hula mbivu endelea kuwa mvumilivu," amesema Mtume Mwingira

"Kama wanasiasa mnatakiwa kulelewa, baba yangu aliniambia usishindwe na mimi nawaambia wanasiasa msitangaze maneno ya kushindwa," amesema

Advertisement

Mtume Mwingira amesema kila aliye mwanasiasa ajue atashinda, kila aliyefika kwenye mkutano huo ajue ameshinda na wenye agenda yakushindwa hawajaja.

"Nimesikiliza maneno yenu ya kisiasa na ya kiserikali, nimeyatunza nimegundua mnahitaji malezi ya kiroho sana ili msiishie njiani," amesema

Kiongozi huyo wa kiroho amesema baada ya kutokea msiba Januari 22, 2020 maono yake kwa bwana yalimuelekeza ibada iwe leo Februari 22,2020 akamshirikisha mke wake.

"Baada ya Msiba huu nilipata maono ya kuzika tarehe ya leo niliwashirikisha ndugu zangu haikuwa rahisi lakini walinielewa," amesema Mtume Mwingira

Awali, akizungumza katika msiba huo, Mbowe aliwaomba watumishi wa Mungu kuliombea Taifa ili haki iweze kutawala katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2020.

Alisema baraka aliyotupa Mungu ya amani, upendo na mshikamano haupaswi kudharauliwa wala kukufuriwa.

"Ombi maalum kwa Mtume Mwingira, ukaungane na watumishi wengine kuliombea Taifa na viongozi kwa kuwa ndiyo wenye uamuzi wote," alisema Mbowe

 

Advertisement