Mwalimu: Kura ndio silaha yako, kutesa kwa zamu

Mwalimu: Kura ndio silaha yako, kutesa kwa zamu

Muktasari:

Mgombea mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu amesema kipindi ambacho wananchi  wanatakiwa ‘kutesa’ ni katika uchaguzi mkuu kwa kuwa ndio wenye ridhaa ya kuamua maisha yao ya miaka mitano ijayo.

Simiyu. Mgombea mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu amesema kipindi ambacho wananchi  wanatakiwa ‘kutesa’ ni katika uchaguzi mkuu kwa kuwa ndio wenye ridhaa ya kuamua maisha yao ya miaka mitano ijayo.

Mwalimu ameeleza hayo leo Jumanne Oktoba 20, 2020 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Busega huku akiwataka kujitokeza kupiga kura kwa wingi kukichagua chama hicho.

"Katiba yetu pamoja na mapungufu yake ya kutoendana na mazingira na mahitaji ya watu wa sasa inatoa nafasi ya watu kutesa kwa zamu na wakati huu wa uchaguzi maana ndio wakati wa wapiga kura kutesa dhidi ya watawala," amesema Mwalimu.

Akiwa katika jimbo la Bukombe aliwaeleza wananchi kuwa kipindi cha uchaguzi si cha kulalamika bali kutuma ujumbe kwa kupiga kura au kutowapigia wagombea husika.

Amesema viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi uliopita hawakuwatendea haki wapiga kura, sasa ni muda wa wananchi kujibu mapigo na sio kulia na kunung'unika.

Mwalimu alidai katika uchaguzi wa mwaka 2020 utakaofanyika Oktoba 28, Chadema kimeishika pabaya  CCM na chama hicho tawala kimepotea.