Mwanafunzi afa ajalini akienda kuripoti shuleni

Tuesday January 14 2020

 

By Stella Ibengwe, Mwananchi [email protected]

Shinyanga. Mwanafunzi Pili Abeid aliyekuwa njiani kwenda shuleni mkoani Dodoma ni kati ya watu wawili waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi, gari ndogo na bodaboda.

Watu wengine 20 walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea jana saa 3:20 asubuhi ikihusisha basi la Kampuni ya Bright Line lililokuwa likitokea jijini Mwanza kwenda jijini Dodoma.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Joseph Kihenge alisema ajali hiyo iliyotokea eneo la kijiji cha Isela wilayani Shinyanga ilitokea baada ya mwendesha bodaboda kujaribu kumkwepa mwendesha baiskeli na kukosa uelekeo kabla ya kugongana uso kwa uso na gari ndogo.

Pamoja na mwanafunzi huyo, mwendesha bodaboda aliyefahamika kwa jina moja la Said naye alifariki dunia papo hapo baada ya kuingia uvunguni mwa basi.

Alisema dereva wa basi la Bright Line aliyetambuliwa kwa jina la George Kessy alikimbia baada ya ajali huku dereva wa gari ndogo naye hajulikani alipo.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga, Dk Rose Malisa alisema maiti ya watu wawili, mwanamke na mwanaume ilipokelewa hospitalini hapo.

Advertisement

“Tulipokea majeruhi 20 wakiwemo watoto mapacha ambao ndugu zao hawajafahamika, baada ya uchunguzi na matibabu, 11 waliruhusiwa kutokana na hali zao kuimarika na waliobaki wamelazwa kwa uchunguzi na matibabu zaidi,” alisema Dk Malisa.

Baadhi ya majeruhi waliolazwa hospitalini hapo ni pamoja na Sophia Ndalawa (20), Eliza Said, Ruthia Timothy, Maria Said (9) na Julius Agustine ambaye yuko chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum. Majeruhi wengine hawajafahamika majina yao.

Advertisement