Mwandishi wosia wa billionea Cohen afunguka

Nairobi. Mwandishi na mtunzaji wa wosia wa Tob Cohen, bilionea wa Uholanzi aliyeuawa nchini Kenya, Chege Kirundi amesema hana lolote la kuficha katika mgawanyo wa mali za mfanyabiashara huyo.

Cohen aliuawa na mwili wake kufichwa katika tanki la maji nyumbani kwake na mkewe anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji hayo.

Kirundi, mwanasheria mkongwe ambaye aliandika wosia wa Cohen amesema ameamua kuutoa mapema kabla ya maziko ya marehemu Jumatatu, kwa kuwa ulikuwa pia na maelekezo ya namna anavyotaka kuzikwa.

“Nimetoa wosia kwa kaka na dada wake Cohen ili waweze kuona matakwa ya marehemu. Chochote watakachofanya juu ya wosia huo ni juu yao, Kirundi amenukuliwa na Gazeti la Sunday Nation la Kenya.

Mwanasheria huyo mwenye uzoefu wa miaka zaidi ya 40, alisema baada ya maziko ya Cohen yaliyomo kwenye wosia huo yanaweza kuwekwa wazi.

“Nilifungua wosia katika ofisi yangu na kuusoma mbele ya Bernard Cohen, kaka yake na dada yake, Gabrielle kama sheria inavyotaka,” alisema Kirundi.

Kuhusu mjane

Kirundi alisema mjane wa marehemu, Sarah Wairimu Kamotho ambaye anashikiliwa katika gereza la lang’ata kwa tuhuma za mauaji ya mumewe, amesema kupitia wakili wake Philip Murgor kuwa atapinga wosia huo katika Mahakama Kuu.

“Namtakia kila la heri katika juhudi zake kupinga wosia wa mumewe,” alisema Kirundi.

Alisema hakuvujisha wosia huo kwa mtu mwingine yeyote isipokuwa kwa wanafamilia wa karibu ambao walitaka kujua mahitaji ya marehemu kuhusu mazishi ya mwili wake.

“Baada ya mazishi yatakayofanyika katika makaburi ya Wayahusi, barabara ya Wangari Maathai, uamuzi utatolewa kuhusu kuuweka wazi wasia huo, lakini kabla ya hapo siwezi kueleza kilichomo,” alisema Kirundi.

Aliongeza kuwa Sarah, mjane wa marehemu aliomba kupitia wakili wake mbele ya Jaji kuwa aachiwe kwa dhamana ili aweze kupigaania haki yake ya mali.

Murgor alisema vyombo vya habari vimeripoti kuwa Cohen amegawa jumba la Milioni 400 za Kenya lililopo Kitisuru kwa dada yake Gabrielle.

Murgor aliongeza kuwa  kwa mujibu wa saraha, asilimia 50 ya jumba la Cohen ni mali yake. Alisema pia kulikuwa na kesi nyingine ya talaka baina ya wanandoa hao na hoja kuu ilikuwa mali.