NBC yazungumzia uboreshaji huduma za bima

Sunday December 22 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) nchini Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Sanlam imezindua kampeni ya bima ya magari ya ‘Ifurahishe gari yako’.

Kampeni hiyo itakayoanza Desemba 2019 hadi Januari 2020 ni sehemu ya malengo ya benki kusogeza huduma zake karibu zaidi na wateja kwa kuwapa mahitaji muhimu.

Akizungumza katika uzinduzi huo mkuu wa kitengo cha bima wa NBC, Benjamin Nkaka amesema kampeni hiyo imezinduliwa katika kipindi sahihi kwa maelezo kuwa kunakuwa na idadi kubwa ya wasafiri.

“NBC imedhamiria kuboresha huduma za bima na kufanya kasi ya matumizi ya bima nchini kuongezeka, kwa kupitia kampeni hii, wateja watakaonunua bima katika matawi ya NBC watapata ofa kadha wa kadha.”

“Ofa  hizo ni huduma ya bure ya mafuta ya kilainishi cha injini na mafuta ya bure kutoka vituo vya mafuta vya Total pamoja na bima ya bure ya ajali ulemavu wa kudumu na gharama za matibabu kutokana na ajali, amesema Nkaka

Meneja mahusiano wa bima wa NBC, Kuruthum Mwaluwinga amesema wamiliki wa magari ya Sh50 milioni na kuendelea watanufaika na mafuta bure pamoja na bima ya bure ya ajali, ulemavu wa kudumu na gharama za matibabu kutokana na ajali.

Advertisement

Amesema wateja wenye magari ya Sh15 milioni hadi Sh49 milioni watapata lita 10 za mafuta bure katika kituo chochote cha Total nchi nzima, bima ya ajali ama ulemavu wa kudumu na gharama za matibabu.

“Wenye magari  ya Sh7 milioni hadi Sh14 milioni watapata lita tano za bure za mafuta katika kituo chochote cha Total nchini, bima ya ajali ya bure ama ulemavu wa kudumu na gharama za matibabu,” amesema.

Advertisement