Phoenix Tanzania yatoa msaada kwa yatima Dar

Phoenix Assurance ambayo ni kampuni ya bima leoJumapili Septemba 22, imetoa misaada mbali mbali pamoja na kushiriki chakula cha mchana na watoto katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Hisani Orphanage Centre kilichopo Mbagala, Dar es salaam .

Msaada huo ni michango kutoka kwa wafanyakazi wote pamoja na nyongeza toka katika kampuni ya Phoenix Tanzania waliojitolea ili kusaidia huduma mbali mbali za kijamii na hasa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Akiongea mara baada ya kutoa msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali watu wa Phoenix Bw Mubaraka Kibarabara alisema licha ya kujihusisha na utoaji wa huduma za bima wameona ni vyema wakajumuika na jamii kwa kuwagusa watoto.

Kibarabara aliongeza:Tunaamini yatima ni sehemu ya jamii yetu tunaahidi kuendelea kuwapa upendo pamoja na kuwafariji. Tulichotoa leo ni kidogo lakini tunaamini kitagusa mioyo yenu,  zaidi mtambue Phoenix Tanzania tuko pamoja nanyi watoto wa Hisani Orphanage Centre.

Akaendelea kusema, tunayo furaha kuweza kuwafikia na kuwahudumia watoto zaidi ya 75 ambao wako kwenye kituo hiki na dhamira yetu ni kuendelea kugusa maisha ya watoto hawa na kuwafanya wajisikie kuwa sehemu ya familia ya Phoenix”.

Naye Meneja wa kituo cha Hisani Orphanage Centre Bi.Hidaya Mutalemwa alishukuru sana kwa msaada huo kutoka Phoenix Tanzania huku akiomba mashirika mengine yaendelee kujitokeza kuwasaidia watoto hao wadogo wanaoshi katika mazingira magumu.

Akiongeza kuwa kituo hicho kinalea watoto ambao ni yatima au wale wenye mzazi mmoja ambae hajiwezi au mwenye ulemavu wa kudumu.

‘Kama unavyoona watoto hawa ni wengi na pia ni wadogo sana kukaa hapa wanahitaji kuhudumiwa, gharama zote  huwa tunatengemea misaada kutoka kwa mashirika mbali mbali na watu binafsi na ndio maana tunashukuru sana Phoenix kwani msaada huu ni muhimu sana kwetu.

Msaada ambao wamepokea leo ni pamoja na madaftari, nguo, chakula ikiwa ni pamoja na mchele, sukari, mafuta ya kupikia, maharage na mahindi.