Polisi Tanzania yazuia mkutano wa Zitto Kabwe

Friday August 16 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalim ya Dar es Salaam nchini Tanzania limezuia mkutano kati ya waandishi wa habari na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ambalo ulitarajiwa kufanyika leo Ijumaa Agosti 16,2019 saa 5 asubuhi.

Polisi waliwasili Makao Makuu ya chama hicho cha upinzani na gari lenye namba za usajili T 863 DFS wakiwa wamevaa nguo za kiraia na kuzuia mkutano huo. Baadaye gari ya polisi walio na sare waliwasili na kumhitaji kiongozi yoyote wa chama baada ya kumkosa Zitto.

"Ndugu waandishi huu mkutano usubiri kwanza, kwa hiyo ninawaomba mtawanyike mara moja," amesema askari mmoja aliyejitambulisha kama RCO wa Kinondoni, John Malulu.

Wakati waandishi wakitawanyika aliwasili Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ambaye wamemchukua kwa ajili ya mahojiano.

Hata hivyo, kabla ya kuchukuliwa na polisi, Ado Shaibu amesema polisi walikwenda nyumba kwa Zitto kumtafuta kwa ajili ya kumhoji.

"Zitto alitaka kuzungumzia kuhusu mkutano wa (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) SADC unaoendelea hapa nchini lakini wameniambia niondoke nao kwenda polisi, hawajaniambia ni kituo gani. Nimewaambia ngoja niweke mambo sawa kisha tuondoke. Hamna haja ya kuwa na wasiwasi," amesema Shaibu.

Advertisement

Polisi wamemchukua Shaibu kwa ajili ya mahojiano. Hata hivyo, polisi hao wamekataa kuzungumza kuhusu sababu za kuzuia mkutano huo.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

Advertisement