Rais mstaafu wa Brazil Lula da Silva atoka kifungoni

Saturday November 9 2019

Rais wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da

Rais wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva 

Brasilia. Rais wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva ametoka Gerezani juzi baada ya kuachiwa huru na mahakama.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Mahakama ya Juu ya Brazil kufuta sheria inayoruhusu washtakiwa waliotiwa hatiani kufungwa, baada ya kushindwa katika rufaa yao ya kwanza.

Kwa Brazil mtu akitiwa hatiani anaweza kukataa rufaa kadhaa kabla ya kuhukumiwa.

Wakati akitoka gerezani Lula alinyanyua mkono na kuonyesha vidole viwili kama alama ya ushindi mbele ya mamia ya wafuasi wake na chama chake cha wafanyakazi, aliokuwa wanapunga bendera na mabango yaliyoandikwa “Free Lula” yakimaanisha mwachie huru Lula.

Aliitisha mkutano Jumamosi mjini Sao Paulo kabla ya kubadili na kuamua kufanya ziara nchi nzima.

Lula alienda jela mwaka 2018 baada ya kuhukumiwa miaka minane na miezi 10 baada ya kupatikana na hatia kwa makosa ya kupokea rushwa kutoka katika kampuni ya ujenzi ili aweze kuipa kandarasi za serikali.

Advertisement

Katika hotuba yake ya kwanza kwa wafuasi wake, Lula aliahidi kupambana kuthibitisha kwamba hakuwa na kosa na kushutumu kile alichoita “upande uliooza wa mfumo wa mahakama”.

Uamuzi wa Mahakama ya Juu wa Alhamisi unaweza kuwanufaisha vigogo wengi walioko magerezani na wengine kwa maelfu

Sheria iliyofutwa ilichangia kufanikisha uchunguzi wa kesi kubwa za rushwa ikiwamo iliyobatizwa kama ‘Car wash’, ambayo ilisababisha vigogo wengi na wanasiasa kwenda jela.

Waendesha mashtaka wamesema hatua hiyo itafanya kazi yao kuwa ngumu kutokana na mlolongo wa rufaa uliopo nchini humo.

Katika tamko lao, wamesema uamuzi wa mahakama hauendi sambamba na nia ya serikali ya kupambana na rushwa.

 

Advertisement