Saa za kampuni ya Green Miles zahesabika Tanzania

Saturday January 18 2020

Mkuu wa wilaya Longido, Frank Mwaisumbe

Mkuu wa wilaya Longido, Frank Mwaisumbe akitangaza kuondolewa rasmi kampuni ya Green Miles kuwinda kitalii wilayani Longido katika mkutano uliofanyika kijiji cha Mundarara Wilaya ya Longido. Picha Mussa Juma 

By Musss Juma ,Mwananchi [email protected]

Arusha. Kampuni ya Green Miles ambayo iliondolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla kumiliki kitalu cha uwindaji cha Lake Natron (East) wilaya ya Longido mkoani Arusha imetakiwa kuondoka katika kitalu hicho ifikapo Jumatatu Januari 20,2020.

Waziri Kigwangalla, Agosti 7 mwaka 2019 alitangaza kuiondoa kampuni hiyo katika kitalu hicho, ambacho kimekuwa na  migogoro baina ya kampuni hiyo na vijiji 23 vinavyozunguka kitalu hicho, halmashauri na serikali wilaya ya Longido na mkoa wa Arusha.

Mkuu wa wilaya Longido mkoani Arusha, Frank Mwaisumbe leo Jumamosi Januari 18, 2020 ametangaza kuondolewa kampuni hiyo ifikapo Jumatatu.

Mwaisumbe amesema kampuni hiyo baada ya kuondolewa na Serikali ya Tanzania mwaka 2019 iliomba kuongezewa muda hadi Desemba 16, 2020 ili ikamilishe uwindaji na kukubaliwa na wizara ya maliasili na utalii.

"Baada ya kuongezwa muda imeendelea kuwapo na sasa Serikali imetoa barua nyingine kupitia katibu mkuu wizara ya maliasili na utalii Profesa Adolf Mkenda ambayo inataka mwekezaji kuondoka ifikapo Jumatatu Januari 20,2020," amesema

Mbunge mstaafu wa Longido, Lekule Laizer amesema wakazi wa Longido wanaipongeza Serikali kwa kumuondoa mwekezaji huyo.

Advertisement

Laizer amesema mwekezaji huyo alikuwa hana mahusiano na vijiji, madiwani na Serikali tangu aanze uwindaji mwaka 2013.

Agosti 14 mwaka 2019, Kamishna wa uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa. Wanyamapori Tanzania  (TAWA), Dk James Wakibara alisema kampuni hiyo ilitakiwa kukamilisha uwindaji kwa wageni ambao tayari walikwishalipia ili kutoathiri watalii  na baadaye ikabidhi kitalu.

'Lile tangazo lilitoka wakati huyu mwindaji alikuwa na commitment za watalii kuja kuwinda hivyo wakipewa muda kukamilisha uwindaji na baadaye kuondoka," amesema

Kwa muda mrefu kulikuwa na mgogoro baina ya kampuni hiyo na vijiji 23 vya Longido ambavyo vimekuwa vikieleza kudai malimbikizo ya madai ya Sh336 milioni .

Hata hivyo,  Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Awadhi Abdalah  amekuwa akipinga madai hayo na kueleza kampuni hiyo haipaswi kulipa huku akisisitiza imekuwa ikifuata taratibu za serikali katika uwindaji.

Advertisement