Safari ya miaka 30 nchi kudai tume huru

Wednesday November 13 2019
pic tume

Wajumbe wa Bunge la Katiba wakitoa maoni yao katika moja ya mikutano ya Bunge hilo mjini Dodoma kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Pamoja na matarajio ya Bunge hilo kuja na mabadiliko kadhaa ikiwamo Tume Huru ya Uchaguzi lakini lilisusiwa na wajumbe kutoka vyama vya upinzani wakiongozwa na vyama vya Chadema na CUF. Picha ya MaktabaKINGO

Ni takribani miaka 30 sasa tangu safari ya wadau kudai tume huru ya uchaguzi nchini ilipoanza.

Kumekuwapo na milima na mabonde katika safari hiyo, wadau wamekuwa wakiibua kilio na kutoweka kulingana na nyakati, lakini zaidi nyakati za uchaguzi.

Licha ya madai hayo kuibuka katika chaguzi zilizopita, wakati huu kilio kimeibuka kwa kasi kutokana na kuwapo kwa kasoro katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

Kutokana na kasoro zilizopo ikiwamo wagombea wa vyama vya upinzani kuenguliwa katika kinyang’anyiro hicho, vyama vitano vimetangaza kujitoa katika uchaguzi huo.

Vyama hivyo ni Chadema, ACT Wazalendo, Chauma, NCCR Mageuzi na UPDP waliotangaza kujitoa jana ingawa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo awali alinukuliwa akisema kuwa ni vyama pekee vimejitoa katika uchaguzi huo na si wagombea wake.

Juzi, Jafo alitangaza kuwarudisha wagombea wote katika mchakato wa uchaguzi huo, ingawa vyama vilivyojitoa vimeshikilia msimamo kuwa havitashiriki katika uchaguzi huo wakidai umegubikwa na hujuma nyingi.

Advertisement

Safari ya kudai tume huru

Safari ya kudai tume huru ya uchaguzi ilianza mwaka 1991 baada ya Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi kuunda tume ya kukusanya maoni kuhusu mfumo wa vyama vya siasa iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo ni kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi.

Jaji Nyalali alionya kuhusu madhara yanayoweza kutokea iwapo taifa lingekosa chombo huru cha kusimamia uchaguzi.

Katika ripoti yake alisisitiza: “Ni lazima muundo wa tume ya taifa ya uchaguzi ubadilike, ili kukidhi haja ya demokrasia ya vyama vingi.”

Jaji Robert Kisanga, aliyeongoza Tume ya Rais ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu maeneo mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi mwaka 1998, alitaja katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kama moja ya mambo ya lazima.

Alisema si sahihi wajumbe wa tume kuteuliwa na Rais ambaye ni kiongozi wa chama cha siasa kinachotawala.

Pamoja na mapendekezo ya tume hizo, serikali haijapata kuyafanyia kazi kwa kuunda tume huru ya uchaguzi.

Tangu wakati huo kumekuwapo na vilio vya wadau kudai tume huru ya uchaguzi ili kuhakikisha kunakuwapo na uwanja sawa kwa wagombea wa vyama vyote vya siasa.

Kitendo cha wadau kuendelea kudai mabadiliko ya tume ni kiashiria kwamba kasoro wanazoziona zinaweza kuondolewa na hatimaye

kufanyika wa uchaguzi huru na wa haki.

Miongoni mwa wadau waliowahi kutoa mapendekezo ya kupatikana Tume Huru ya Uchaguzi ni Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata).

Walipendekeza muundo wa tume uakisi majukumu yake, kwa kuwezesha kuwapo kamisheni itakayoongoza Tume hiyo katika utendaji kazi wake, na kuwajibika kwa mambo yote ya kisera na kimaamuzi, pamoja na kuundwa kwa sekretarieti ya Tume itakayokuwa chini ya Mkurugenzi wa Tume, kama Mtendaji Mkuu.

Kutokana na Rais anayekuwa madarakani, kuwa miongoni mwa wagombea au kiongozi wa chama kimojawapo cha siasa kinachosimamisha mgombea, Jukata walishauri kupunguzwa kwa mamlaka ya Rais ya uteuzi, tofauti na sasa ambapo mamlaka yote ya uteuzi yako chini yake.

Pia walipendekeza mchakato wa kuwapata makamishna wa tume utangazwe, ufanyike usaili, kisha majina hayo yafanyiwe mchujo na kupatikana majina 20, yatakayopelekwa kwa Rais ambaye atapendekeza majina tisa yatakayopelekwa bungeni kufanyiwa uchambuzi, kujadiliwa na kisha yawasilishwe tena kwa Rais ili amteue mwenyekiti wa Tume hiyo.

Baada ya uteuzi huo atayawasilisha majina hayo kwa Jaji Mkuu ambaye atayatangaza na kuwaapisha makamishna wa Tume. Pia Rais atamteua Mkurugenzi wa Tume kutokana na majina mawili yatakayopelekwa kwake na Tume ya Uajiri wa Umma kutokana na mchakato huru na wa wazi wa uajiri.

Njia hiyo inaweza kupunguza malalamiko dhidi ya Tume, kwa sababu mchakato utakuwa umepitia taratibu za kawaida za kuajiri, na kupunguza nafasi ya uteuzi kwa Rais.

Katika kuendeleza madai ya kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi, mwanzoni mwa mwaka huu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilisema kitaandaa rasimu ya muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi ili ijadiliwe kabla ya uchaguzi mkuu 2020.

Kaimu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alikaririwa akisema kuna haja ya kufanya marekebisho katika tume ya uchaguzi ikiwemo kubadili vifungu vya Katiba vinavyohusiana na tume, sheria ya uchaguzi ya mwaka 2002 pamoja na kanuni za uchaguzi wa urais na ubunge ili kuwa na uchaguzi huru na haki.

Amesema chama hicho kina azma ya kuhakikisha wanapatikana washindi wa kweli katika chaguzi ili kuondokana na suala la kulinda kura baada ya kukamilika kwa zoezi la kupiga kura.

Pia Baraza la Wazee wa Chadema lilisisitiza kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi katika chaguzi zote zijazo.

Julai mwaka huu, Mwenyekiti wa baraza hilo, Hashim Juma Issa alisema tume hiyo itasaidia kuwepo kwa uchaguzi huru wa watu kuchagua chama wanachotaka.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Mwaka 2012, Serikali ya awamu ya nne iliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba ambayo miongoni mwa mambo waliyopendekeza kuwapo katika katiba mpya ni Tume Huru ya Uchaguzi.

Katika rasimu ya kwanza na ya pili kulikuwapo na mapendekezo ya Tume Huru ya Uchaguzi ambayo ingesimamia na kuratibu shughuli za uchaguzi na masuala yanayohusu vyama vya siasa.

Kwamba tume hiyo iundwe na mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wengine saba watakaoteuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na kamati ya uteuzi.

Mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watashika madaraka mara baada ya kuthibitishwa na Bunge.

Miongoni mwa sifa za mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ni mtu aliyewahi kushika wadhifa wa Jaji wa Makakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu na ameshika wadhifa huo kwa kipindi kisichopungua miaka mitano.

Hata hivyo mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya ulisimama tangu mwaka 2015 ukibaki hatua ya kupigiwa kura na mpaka sasa hakuna kinachoendelea.

Tangu wakati huo wadau mbalimbali walipaza sauti kutaka mchakato huo uliogharimu mabilioni ya fedha kuendelea, lakini mpaka sasa kumekuwa kimya.

ZEC

Baada ya kupatikana maridhiano visiwani Zanzibar mwaka 2010, Serikali iliunda Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) iliyokuwa na wajumbe kutoka pande mbili za vyama vya siasa.

ZEC iliundwa kwa wajumbe wawili kutoka CCM na wawili kutoka CUF na mmoja kutoka chama cha Sauti ya Umma (Sau) pamoja na wajumbe ambao hawatokani na vyama vya siasa.

Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti Jecha Salim Jecha, mwaka 2015 ilifuta matokeo ya uchaguzi kwa madai ya kuwapo ukiukwaji mkubwa wa taratibu na kasoro nyingi.

Baada ya Jecha kufuta matokeo ya Urais wajumbe hao waligawanyika huku wa kutoka CUF wakidai hawakushirikishwa katika uamuzi huo.

Jecha alifuta matokeo hayo na kutangaza kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao ulisusiwa na CUF.

Maoni ya wadau

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa anapendekekeza kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ili kuondoa misuguano inayojitokeza mara kwa mara nyakati za uchaguzi.

Anasema hata uchaguzi wa serikali za mitaa unapaswa kusimamiwa na tume huru kwa kuwa unaposimamiwa na chombo cha serikali ni rahisi kutokea malalamiko kwa kuwa nayo ina maslahi.

“Si sahihi Tamisemi kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa nayo ina maslahi, hivyo kutokea kwa mgogoro. Kuwepo kwa tume huru ambayo itakuwa na ofisi kila wilaya pamoja na watumishi wake,” anasema.

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anasema msimamo wa chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na chaguzi zijazo ni kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi ili uchaguzi wa 2020 usiwe na dosari kama zilizotokea sasa.

“Bila Tume Huru ya Uchaguzi pasiwe na uchaguzi wowote nchini. Viongozi wa kitaifa wa vyama watoke na tamko la pamoja kutaka Tume Huru ya Uchaguzi,” anasema Zitto.


Advertisement