Serikali ya Tanzania yaomba muda zaidi maombi wadhamini wa Lissu

Friday February 21 2020

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam . Upande wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili  aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu umeomba muda wa kutosha  kupitia na kujibu  maombi ya kujitoa kwa  wadhamini wa  makamu mwenyekiti huyo wa Chadema.

Maombi hayo yamewasilishwa leo Ijumaa Februari 21, 2020 na wakili mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon.

Lissu na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka matano  likiwemo la uchochezi, hajatokea mahakamani tangu aliposhambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 mjini Dodoma.

Siku hiyo alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Dodoma na usiku akahamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na baadaye kwenda Ubelgiji kumalizia matibabu. Lissu amepona lakini bado yupo nchini Ubelgiji kwa maelezo kuwa anataka kuhakikishiwa usalama wake kabla ya kurejea Tanzania.

Kutoonekana kwake mahakamani kumesababisha shauri hilo kuzorota huku  wadhamini wake wakiomba kujitoa.

Maombi hayo yaliwasilishwa jana Alhamisi Februari 20, 2020 na mmoja wa wadhamini hao, Robert Katula aliyeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa hati ya kumkamata Lissu, baada ya jitihada za kumtafuta kushindikana.

Advertisement

Leo Ijumaa Februari 21, 2020 wakili huyo wa upande wa mashtaka alieleza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kutokana na wadhamini wa Lissu kuwasilisha maombi hayo, hawakupata muda mzuri wa kuyapitia.

"Hivyo, kwa sababu hiyo tunaiomba mahakama itupe muda wa kutosha wa kupitia maombi hayo ili na sisi tuweze  kuandaa kiapo kinzani na kuwasilisha mahakamani hapa.”

"Katika maombi ya wadhamini, wameweka vitu vingi, hivyo kama upande wa mashtaka tunahitaji tupewe muda wa kutosha ili tuweze kupitia maombi yao,” amesema.

Wakati upande wa mashtaka ukiomba muda zaidi ili uweze kupitia maombi ya wadhamini hao, wakili wa Lissu aliiomba mahakama hiyo iahirishe kusikiliza maombi hayo hadi Februari 24, 2020.

Akimwakilisha Peter Kibatala, wakili Rwekama Rwekiza amesema kwa kuwa Kibatala  yupo Mahakama ya Rufani katika kesi nyingine, anaomba iharishwe kwa muda mfupi hadi Jumatatu, siku ambayo atakuwepo.

Lakini baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo la hadi Machi 10, 2020.

Desemba 19, 2019 Mahakama hiyo ilitoa amri kwa wadhamini hao kuhakikisha Lissu, ambaye pia ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea, anafika mahakamani.

Januari 30,2020 Katula aliieleza mahakama kuwa juhudi walizofanya ni pamoja na kuwasiliana na mshtakiwa mwenyewe bila mafanikio pamoja na kumuandikia barua mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwasaidia ili arejee nchini.

Katula amedai kuwa wamefanya jitihada za kumleta Lissu nchini kwa nguvu zao zote, lakini imeshindikana hivyo wanaiomba mahakama itoe kibali cha kukamatwa kwake.

Katika kesi ya msingi Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano, likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.

Advertisement