Serikali ya Tanzania yatangaza mkakati mpya ununuzi wa korosho

Friday September 20 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Japhet Hasunga leo Ijumaa Septemba 20, 2019 ametangaza mfumo mpya wa ununuzi wa korosho kwa mwaka 2019/20 utakao kuwa katika minada wa wazi utakaokuwa katika Jukwaa la soko la bidhaa (TMX).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Hasunga amesema katika mfumo mpya utakaoanza rasmi Septemba 30, 2019 wakulima wote watasajiliwa na Bodi ya Korosho kupitia mfumo wa wizara ya kilimo wa kusimamia biashara za Kilimo (ATMIS).

 "Tutaendesha minada ya wazi, kila Mtanzania anaweza kuona na kushiriki na watu kote duniani watashiriki. Wanunuzi walisajiliwa na kukidhi vigezo watatakiwa kulipa kinga ya dhamana kutegemea kiasi cha korosho mnunuzi anachotaka," amesema Hasunga.

Akifafanua zaidi, Waziri Hasunga amesema mfumo huo una tofautiana na minada ya awali ambapo wanunuzi walikuwa wakiweka zabuni zao kwenye sanduku kisha linafunguliwa.

"Mtu yoyote anayetaka kununua korosho ataingia kwenye tovuti ya wizara na kuweka kiasi anachohitaji. Mpaka sasa tuna watu wengi, tuna kampuni nyingi zimejisajili," amesema.

Amesema wanunuzi wa ndani na nje wataruhusiwa kununua korosho kwa mafungu kati ya tani 50 mpaka 500 kulingana na mahitaji.

Advertisement

Amesema katika msimu huu, Tanzania inatarajia kuvuna tani 300,000 za korosho kutoka na kuongezeka kwa uzalishaji.

Kuhusu msimu uliopita amesema kati ya tani 224,000 zilizokusanywa, Serikali imeshalipa Sh723 bilioni huku zaidi Sh50 milioni zikiendelea kulipwa.

Advertisement