Simba watishia amani kijiji cha Nyichoka

Muktasari:

Wakazi wa kijiji cha Nyichoka kata ya Kyambahi wilayani Serengeti wameanza kuwa na hofu kutokana na simba kula mifugo yao mara kwa mara.

Serengeti. Wakazi wa kijiji cha Nyichoka kata ya Kyambahi wilayani Serengeti wameanza kuwa na hofu kutokana na simba kula mifugo yao mara kwa mara.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 3, 2019 ofisa mtendaji wa kata hiyo, Mohammed Hamisi amesema, "kwa mwezi Novemba hadi sasa wameshakula ng'ombe 19, mbuzi 26, kondoo 30 na nguruwe mmoja katika vijiji vya Nyichoka na Bukore.”

Amesema askari walifika na kufanya tathmini, “wananchi wanafanya msako vichakani lakini kila siku usiku lazima simba waje kula mifugo.”

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu ameagiza taasisi zote za uhifadhi kushirikiana kuwaondoa simba hao aliodai wapo kundi ili kutoendelea kuleta madhara kwa mifugo na wananchi.