Advertisement

Nsa Kaisi afariki dunia

Thursday February 13 2020
Nsa puic

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Nsa Kaisi amefariki dunia leo Alhamisi Februari 13, 2020.

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Nsa Kaisi amefariki dunia leo Alhamisi Februari 13, 2020 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kaisi aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwa ni pamoja na mkuu wa Wilaya, Mkoa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza alichaguliwa kuwa mshauri wa masuala ya siasa wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Februari 13, 2020, Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, Profesa Mark Mwandosya amethibitisha kifo cha mwanasiasa huyo ambaye pia alikuwa mwanahabari, na kwamba alimfahamu kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.

“Ni kama kaka kwangu, tunatoka eneo moja, ukitaja Rungwe na Kyela ni kama unataja eneo moja. Juzi (Jumanne) alikimbizwa hospitalini na taarifa nilizonazo amefariki usiku wa kuamkia leo,  mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Lugalo,” anasema Profesa Mwandyosa.

Amesema msiba upo nyumbani kwake Oysterbay  na kwamba mwili wake utaagwa Jumamosi katika Kanisa la Kiinjili la Kirutheni Tanzania (KKKT)- Azania Front, kisha kusafirishwa kwenda Kyela, Mbeya kwa  mazishi.

Amesema Kaisi aliwashughulikia  wahujumu uchumi wa Mkoa wa Kagera alikowahi kuwa mkuu wa mkoa, ni kati ya mambo yanayomuwekea rekodi mwanasiasa huyo.

Advertisement

“Maadui walimchukia lakini alijipatia sifa nyingi Serikalini na baada ya hapo aliingia jeshini,” amesema Profesa Mwandosya.

Profesa Mwandosya amesema Kaisi aliyewahi kufanya kazi katika gazeti la Uhuru na Nationality akiwa chini ya Mhariri Mtendaji Rais mstaafu Mkapa amesema, “gazeti la Nationality lilikuwa la kipekee, lilikuwa la msimamo wa Tanu na lilikuwa kwa ajili ya wasomaji wa Kiingereza wa nje na ndani ya nchi, ilikuwa forum ya wapigania uhuru kusini mwa Afrika.”

Amesema Kaisi ni kati ya watu waliokuwa na misimamo na walitumia kalamu zao ipasavyo.

Advertisement