Takukuru yaanika miradi yenye viashiria vya rushwa

Friday July 12 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected] co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, Theresia Mnjagira  amesema miradi 16 ya maendeleo ya Sh40 bilioni walioifanyia ukaguzi, nane imebainika kuwa na viasharia vya  rushwa.

Mnjagira ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 12, 2019  wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni, 2019 na kwamba miradi hiyo inatekelezwa Wilaya ya Ubungo na Kinondoni.

Ameitaja miradi  yenye viashiria vya rushwa ina thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni,  ikiwemo ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Kimara, ujenzi wa maktaba, jengo la utawala na maabara na ukarabati wa madarasa manne  na ofisi ya walimu ya shule ya msingi Kulangwa.

"Kwanza taratibu za manunuzi kutofuatwa, fedha kutotolewa kwa utaratibu. Tumeshaanza uchunguzi ili kubaini ukiukwaji wa taratibu hizi na ikithibitika hatua stahiki zitachukuliwa," amesema Mnjagira.

Mnjagira amesema mojawapo ya majukumu ya Takukuru ni kufuatilia matumizi ya fedha za umma  kuhakikisha  miradi inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa  na thamani ya fedha iliyokusudiwa inapatikana.

Advertisement