Takukuru yaeleza ilivyomkuta gesti mhadhiri NIT akiomba rushwa ya ngono

Wednesday October 9 2019

Mhadhiri wa chuo cha usafirishaji (NIT) Samson

Mhadhiri wa chuo cha usafirishaji (NIT) Samson Mahimbo  

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Takukuru leo Jumatano Oktoba 9, 2019 imeieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi ilivyomkuta katika nyumba ya kulala wageni mhadhiri msaidizi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo (68) akiwa mtupu.

Mahimbo anakabiliwa na kesi ya  kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa chuo hicho, Victoria Faustine.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Oktoba 9, 2019 na wakili wa taasisi hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania,  Faraja Salamba wakati akimsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi.   

Salamba amedai wakati wa tukio hilo mhadhiri huyo alikuwa mwajiriwa wa NIT akifundisha wanafunzi wa muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka  2015/2016 somo la usimamizi wa barabara na usafirishaji.

Amedai Januari 5 na 11, 2017 mshtakiwa alitumia madaraka yake vibaya kwa kuomba rushwa ya ngono na alimpigia simu Victoria na kumsisitiza wakutane katika baa ya Shani.

Amedai walipokutana mshtakiwa huyo alikuwa na mtihani wa Victoria wa marudio wa somo alilokuwa akimfundisha na majibu, alimpa aufanye na alipomaliza akasahihisha na kumpa alama 67.

Advertisement

Imedaiwa kuwa baada ya Victoria kumaliza kufanya mtihani huo na kusahihishiwa walihamia baa nyingine ya Camp David na kunywa pombe na mshtakiwa kuchukua chumba.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa walipoingia chumbani mshtakiwa alivua suruali na kupaki na nguo ya ndani na kumkumbatia mwanafunzi huyo.

Salamba amesema wakati mhadhiri huyo akimvua nguo mwanafunzi huyo mlango uligongwa na Victoria alikwenda kufungua na waliingia maofisa wa Takukuru

“Waliingia maofisa wa Takukur, mjumbe na mhudumu wa Baa na kukuta nguo za mshtakiwa juu ya meza,” amesema Salamba.

Wakili huyo wa Takukuru amedai  Januari 12 ,2017 mshtakiwa huyo aliandika maelezo Takukuru na Agosti 14, 2019 alifikishwa mahakamani.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka unatarajia kuita mashahidi sita na kuwasilisha vielelezo saba.

Baada ya kusomwa kwa maelezo hayo, mshtakiwa alikubali maelezo yake na kukana shtaka linalomkabili.

Kesi itaanza kusikilizwa Novemba 4, 2019 kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo mhadhiri huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 12, 2017 katika nyumba ya kulala wageni ya Camp David iliyopo Mlalakuwa Mwenge.

Ilidaiwa akiwa mwajiriwa wa NIT kozi ya usimamizi wa barabara na usafirishaji namba LTU 07101 kwa kutumia mamlaka yake alimlazimisha mwanafunzi huyo kutoa rushwa ya ngono.

Anadaiwa kuomba rushwa hiyo ili aweze kumfanya mwanafunzi huyo kufaulu mtihani wake wa marudio katika kozi ya usimamizi wa barabara na usafirishaji uliokuwa unafanyika Januari 5, 2017.

Mshtakiwa  huyo yupo nje kwa dhamana na alikana mashtaka yanayomkabili.

Advertisement