TanTrade yadadavua ajira zilizopatikana kwenye maonyesho ya biashara mwaka huu

Wednesday November 27 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TanTrade), imebainisha kwamba ajira za muda mfupi 14,912 zilipatikana kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Novemba 27, 2019 jijini Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Mohammed Hamis wakati akieleza mafanikio ya mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano.

Amezitaja ajira zilizopatikana kuwa ni pamoja na ujenzi, ulinzi na usafi huku mauzo ya papo kwa hapo kwenye maonyesho hayo yakiwa ni zaidi ya Sh209.4 milioni.

Amesema Kampuni 437 zilipata oda ya kufanya biashara (Business deals) zenye thamani ya Sh7.93 bilioni.

“TanTrade imeendelea kuratibu Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa lengo la kutoa fursa za kutangaza bidhaa zilizoongezwa thamani na upatikanaji wa teknolojia ili kupanua wigo wa masoko ya nje ya nchi,” amesema Hamis.

Amesema maonyesho hayo yalivutia watembeleaji 260,037 kutoka ndani na nje ya nchi huku upatikanaji wa mapato ya Serikali kutokana na kodi mbalimbali ikiwemo VAT, ushuru wa forodha na kodi ya uingizaji bidhaa zikiongezeka.

Advertisement

Mkurugenzi huyo amebainisha kwamba kila mwaka TanTrade inaratibu ushiriki wa kampuni za Tanzania katika maonesho ya nje nchi hususan zile zilizo na utengamano na Tanzania kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo wastani wa kampuni 200 hushiriki.

“Mwaka 2018/19, TanTrade iliratibu maonesho ya 15 ya Biashara China (Asean Expo 2018). Kampuni 20 zilishiriki na zilitafutiwa masoko ya bidhaa na kutangaza bidhaa na vivutio mbalimbali vya uwekezaji ikiwemo vivutio vya utalii, mazao ya kilimo hususan kahawa, chai, karafuu, asali, korosho, mazao ya jamii ya kunde na bidhaa za mikono kama vile vikoi,” amesema.

Advertisement