Upelelezi kesi ya Dk Tenga na wenzake wakamilika

Muktasari:

Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa kampuni ya mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili Dk Ringo Tenga, umekamilika


Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa kampuni ya mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili Dk Ringo Tenga, umekamilika.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatano Julai 17, 2019, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Simon alieleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kuandaa nyaraka muhimu kuhusu kesi hiyo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha  kesi hiyo hadi  Julai 26, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wote wamerudishwa rumande.

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni mhandisi,  Hafidhi Shamte, mkurugenzi mkuu wa kampuni wa hiyo;  mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni; mkuu wa fedha wa kampuni hiyo,  Noel Chacha na kampuni ya Six Telecoms.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Novemba 20, 2017 kujibu mashtaka sita yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Katika kesi ya msingi, Dk Ringo ambaye ni Mkurugenzi na Mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadai kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14,2016 Dar es Salaam, walitoza maalipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa  chini ya kiwango cha Dola za Marekani  0.25 kwa  dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini(TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao , wanadaiwa  katika kipindi hicho  walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Dk Tenga  na wenzake wanadai kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14,2016 maeneo ya Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola 0.25 za Marekani kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida kinyume cha sheria.

Pia katika kipindi hicho wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa Dola 3,282,741.12 za Marekani kwa TCRA kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola 466,010.07 za Marekani kwa TCRA.

Katika shtaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni,Dk Tenga na Chacha wanadaiwa kuwa, walitumia ama walisimamia Dola 3,282,741.12 za Marekani wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashitaka yaliyotangulia.

Vile vile, washitakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola  3,748,751.22 za Marekani (sawa na Sh. 8 bilioni ).