Usalama taarifa binafsi shakani

Friday February 21 2020

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Usajili wa taarifa za watu kwa mfumo wa kidigitali, umeanza kuibua wasiwasi wa usalama wa taarifa binafsi, hivyo kuibua hoja ya umuhimu wa kuwapo sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi na faragha nchini.

Hoja ya kutungwa kwa sheria ya aina hiyo, imepata nguvu hasa baada ya uamuzi wa serikali kusajili simu kwa kutumia kitambulisho cha taifa.

Kufuatia kilio hicho, Serikali imeeleza kuwa ipo katika mchakato wa kuandaa sheria hiyo ya kulinda taarifa binafsi za watu.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alikiri kuwapo kwa hatari ya ukiukwaji katika matumizi ya taarifa binafsi, lakini akasema muda umefika wa kuwa na sheria inayolinda taarifa binafsi licha ya kuwapo kwa baadhi ya masharti katika sheria nyingine.

Kitambulisho cha taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), mbali na kutumika kusajili simu, pia kinatumika kuwezesha huduma nyingine kama vile za pasipoti, leseni na ulipaji wa kodi.

Hata hivyo, baadhi ya watu wameibua hoja kuhusu ulinzi na usalama wa taarifa za watu zilizokusanywa na Nida, dhidi ya matumizi yake.

Advertisement

Hofu ya usalama wa faragha ya mawasiliano, inachagizwa na tukio la hivi karibuni la kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa sauti za badhi ya viongozi wastaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wabunge wa chama hicho na kuwasababishia kuingia matatani na viongozi wao.

Sauti hizo ni za makatibu wakuu wastaafu wa CCM; Abdulrahman Kinana na Yussuf Makamba pamoja wa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe. Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba na wabunge Nape Nnauye (Mtama) na William Ngeleja (Sengerema).

Vigogo hao walijikuta wakiingia matatani kwenye uongozi wa chama chao kutokana na mazungumzo yao kusikika wakimteta mwenyekiti wa chama hicho na kuzungumzia kuwepo kwa mpasuko ndani ya chama.

Nnauye, Makamba (ambaye alipoteza nafasi yake ya uwaziri katika sakati hilo) na Ngeleja walisamehewa baada ya kuomba radhi huku Membe, Kinana na Makamba wakisubiri hatima yao kuamuliwa na vikao vya juu vya CCM.

Julai 30, 2019, Kampuni ya Simu ya Vodacom Tanzania ililazimika kutoa taarifa kwa umma ikieleza jinsi inavyolinda taarifa za wateja wake, baada ya kuwapo malalamiko dhidi yake katika mitandao ya kijamii.

Kutokana na malalamiko hayo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), katika taarifa yake, ulipendekeza kwa serikali kwamba itungwe sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi (Data Protection and Privacy Act) ili kuepusha ukiukwaji wa haki ya faragha kama inavyotolewa na Katiba ya nchi.

Kauli za wananchi na wadau

Mfanyabiashara na mkazi wa Segerea, Dar es Salaam, Abdulfatah Lyeme amesema ana hofu kwamba washindani wake kibiashara wanaweza kufuatilia taarifa zake na kumwangamiza sokoni kwa fitina.

Lyeme anasema awali ilikuwa ngumu lakini utoaji wa taarifa za kina kwa mfumo wa vidole , unaweka rehani taarifa binafsi kwani ni vigumu kutambua nani mwenye nia ovu au njema katika taasisi zinazochukua taarifa hizo.

“Mtu anaweza kuchukua taarifa zako akauza kwa wabaya wako, hana hasara na wala hutamfahamu, kwa hiyo hili linahitaji kutazamwa sana,” anasema Lyeme.

Mratibu THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa hatofautiani sana na Lyeme, akisema kutokana na urasimishaji wa taarifa nyingi kwenye mfumo huo kwa sasa, ni muhimu kuwa na sheria hiyo.

Wakili wa Kujitegemea, Daimu Halfan alisema pamoja na umuhimu wa kuanzisha sheria ya kulinda taarifa za watu, ni muhimu kuimarisha uwezo wa mifumo ya ndani, uadilifu wa watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu pamoja na uhakika wa Serikali katika ulinzi wa taarifa za mtu binafsi.

“Kuna watumishi si waaminifu, hata polisi, mkurugenzi wa mashitaka au Takukuru wanapokuwa na mamlaka kisheria kuchukua taarifa hizo, kwa hiyo wadhibiti kwanza mifumo ya ndani, halafu sheria hiyo ikishapitishwa kianzishwe chombo cha mlalamikaji atakayelipwa hata fidia ya athari atakazopata,” alisema Halfan.

Wakili mwingine wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema pamoja na uwepo wa vifungu vya vya kulinda taarifa binafsi, wakati mwingine kumekuwa na ukiukwaji wa haki ya faragha na uvujishaji wa makusudi wa taarifa hizo, hali inayoleta madhara kwa watumiaji.

Alisema sheria mpya inahitajika ili kuweka msingi utakaolazimisha taasisi za umma kupata kibali cha mahakama pale inapohitajika ushahidi wa sauti, au taarifa za data kutoka kampuni za simu nchini.

Kuingiliwa kwa taarifa

Kuingiliwa na kufuatiliwa kwa mawasiliano ya watumia simu za mawasiliano, kunazungumziwa pia na Kampuni ya Vodafone/Vodacom (duniani) ambayo ambayo kupitia taarifa zake imekuwa ikiweka wazi jinsi serikali mbalimbali duniani zinavyoingilia mawasiliano ya watu wake.

Taarifa hizo zinapatikana katika taarifa ya Vodacom juu ya sheria za utoaji taarifa (Law Enforcement Disclosure Report) zinagusa nchi 29 ambako kampuni hiyo inafanya kazi zake.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa nchi nyingi hutaka taarifa za watumiaji wa huduma za mawasiliano wakati mwingine bila vibali vya kisheria, huku wengine wakifuatilia na kusikiliza mazungumzo ya watumiaji wa huduma zao, kufuatilia walipo na kuagiza nakala ya ujumbe wa mawasiliano.

Ripoti ya mwaka 2013 inaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa inaongoza kwa kudai taarifa katika nchi nane za Afrika ambako Vodacom inafanya kazi.

Mwaka huo Vodafone walipokea maagizo yapatayo 100,000 kutoka serikali za nchi za Afrika zikitaka taarifa mbalimbali za baadhi ya wateja, zikiwamo namba za simu, anuani zao, eneo kifaa cha mawasiliano kilipo (device location), muda wa kuongea na ujumbe wa maandishi.

Taarifa hiyo inaitaja Tanzania kuwa inaongoza kwa kuagiza taarifa nyingi zaidi kuliko nchi nyingine Afrika, ikitoa mfano kwamba iliagiza taarifa karibu mara elfu moja, wakifuatiwa na DRC (496) na Lesoto (488). Vodafone pia wanatoa huduma katika nchi za Afrika Kusini, Msumbuji, Kenya (kama Safaricom), Misri na Ghana.

Maandalizi ya sheria

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alisema tayari wizara imeanza maadalizi ya kutunga Sheria ya Kinga ya Taarifa Binafsi (Transfer Personal Data Orotection Act), itakayohusisha ulinzi wa data zote zikiwamo alama za vidole kwa taasisi yoyote itakayochukua taarifa hizo kwa matumizi yoyote.

Nchini Uganda tayari kuna Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha ya mwaka 2019, kifungu cha 10 kinalinda faragha na taarifa binafsi za watu.

“Kwa mfano ukiacha taarifa zako hotelini Mwanza kwa alama ya vidole, tuhakikisha zinalindwa kisheria, taasisi za umma zitakazohitaji taarifa kupitia mfumo huo, zitalazimika kisheria kulinda na kuhifadhi, ukiweka alama za kidole kituo cha Polisi taarifa zako zilindwe,” alisema Nditiye.

Nditiye alisema kuwa sheria iko wazi, atakayekiuka atachukuliwa hatua na kwamba tayari ukusanyaji wa maoni ya wadau umeishaanza ili kupate rasimu ya kwanza.

Sheria zinazogusa uhifadhi wa taarifa

Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015 inalipa Jeshi la Polisi madaraka ya kufanya upekuzi na kuchukua vifaa vya mawasiliano bila kibali cha mahakama hata pale ambapo haki za wengine hazijakiukwa au maslahi ya umma.

Hata hivyo, sheria hiyo hiyo kifungu cha (7) kinakataza uingiliwaji wa taarifa binafsi kama ilivyo katika Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016.

Pili, Kanuni ya 6 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2018 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 zinaweka wajibu wa utunzaji wa siri kwa wamiliki wa mitandao au waendeshaji wa mitandao, mawakala na wateja na kukataza utoaji wa taarifa bila kibali.

Mipaka ya Haki ya Faragha imetolewa chini ya Kifungu cha 29(5) cha Katiba kinachosema; ‘‘Ili watu wote waweze kufaidi haki na uhuru ilivyotajwa na Katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma”

Advertisement