Utata Arusha mwanafunzi aliyejiua kwa risasi

Tuesday August 20 2019

Kamanda polisi mkoa  Arusha,,Mwanafunzi kidato , nne, Shule ya Sekondari, Arusha Meru,Faisal Salimu, Jonathan Shani

 

By Waandishi wetu, Mwananchi [email protected]

Arusha. Utata umezingira kifo cha mwanafunzi wa kidato cha tano wa Shule ya Sekondari ya Arusha Meru baada ya kukutwa chumbani kwake akiwa amefariki kwa risasi iliyompiga usoni kwake.

Habari za awali zinasema mwanafunzi huyo, Faisal Salum alijipiga risasi kwa kutumia bunduki aina ya Rifle Winchester inayomilikiwa na baba yake, wakati akiwa chumbaji alfajiri ya kuamkia juzi.

Jeshi la Polisi limesema linaishikilia bunduki hiyo kwa uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kutaka kujua kama inamilikiwa kihalali na linaendelea na uchunguzi zaidi wa kifo hicho baada ya Faisal kutoacha sababu za uamuzi wake.

Mtoto huyo alikuwa akiishi na baba yake, Salim Ibrahim (59) katika nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) zilizoko eneo la Soko Kuu jijini Arusha.

Wawili hao walikuwa wakiishi pamoja baada ya baba yake kuachana na mkewe ambaye aliolewa na mwanaume mwingine.

Akizungumza na Mwananchi jana, kamanda wa polisi Arusha, Jonathan Shana alisema polisi walimhoji Ibrahim kuhusu tukio hilo na baadaye kumuachia.

Advertisement

“Baada ya uchunguzi wa awali, tumemuachia ila uchunguzi unaendelea,” alisema Kamanda Shana.

Jana, Shana alisema polisi wanaendelea kuchunguza kisa hicho na bunduki aliyotumia kujipiga risasi nayo wanaishikilia kwa uchunguzi zaidi.

“Tunafuatilia kama ilikuwa inamilikiwa kihalali ama la, lakini pia tunachunguza tukio hili kama silaha ilikuwa imehifadhiwa sehemu salama,” alisema Kamanda Shana.

Baada ya tukio hilo, polisi walisema uchunguzi wa awali umebaini mwanafunzi huyo alikuwa anasumbuliwa na msongo wa mawazo kutokana na kushutumiwa kuwa anatumia dawa za kulevya.

Lakini majirani wanasema walikuwa wakimuona kijana huyo akitoka asubuhi na kurejea jioni.

Mmoja wa majirani wa nyumba ya familia hiyo, Juma Rashid aliliambia Mwananchi kuwa hajui chanzo cha mtoto huyo kujiua.

“Huyu kijana alikuwa anaishi na baba yake baada ya kuachana na mama yake aliyeolewa na mwanaume mwingine. Sasa haijulikani nini chanzo,” alisema Rashid.

Jirani mwingine anayefanya biashara karibu na nyumba hiyo iliyo Kiwanja Namba 3, Minja alisema maisha ya familia ya baba na mtoto huyo yalikuwa hayajulikani sana.

“Huyu mzee ni mfanyabiashara, ana duka lake na huyu mtoto alikuwa akionekana jioni hapa na kutoka asubuhi. Hadi leo (juzi) amefariki sisi hatuna taarifa,” alisema.

Juhudi za kumpata baba yake, hazikufanikiwa.

“Tumepata taarifa kuwa mtoto amezikwa jana na inaonekana hapa nyumbani hakuna msiba, labda upo kwa mama yake,” alisema Minja.

Mwananchi ilishuhudia nyumba ya baba na mtoto huyo ikiwa imefungwa huku baadhi ya majirani wakionekana kushangazwa na tukio hilo.

Shule alikosoma haina taarifa

Hata uongozi wa Shule ya Arusha Meru haukuwa na taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo.

“Sisi hatuna taarifa, tumesoma kwenye vyombo vya habari,” alisema mkuu wa shule ya Arusha Meru, Mustapha Nassoro jana.

“Lakini huyu kijana alikuwa anasoma hapa kidato cha tano na aliandikishwa shuleni hapa na mama yake.”

Hata hivyo, alisema wanafuatilia na watatoa taarifa Jumatano baada ya kuonana na familia.

“Kwa sasa kama uongozi wa shule hatuna cha kusema, ila Jumatano labda tutazungumza baada ya kuonana na familia,” alisema mwalimu huyo.

Tukio kama hilo liliwahi kutokea mwaka 2012 wakati mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Edmubdrise, John Justine (17) alipojiua kwa kutumia bunduki ya baba yake mzazi aina ya shotgun.

Imeandikwa na Mussa Juma, Mohamed Kaoneka, Teddy Kilanga na Elizabeth Elias


Advertisement