Viongozi Afrika watakiwa kujitathmini mapambano dhidi ya Ukimwi

Tuesday December 3 2019

Rais wa Rwanda, Paul Kagame na mkewe Jeannette

Rais wa Rwanda, Paul Kagame na mkewe Jeannette Kagame wakifiatilia uzinduzi wa mkutano wa 20 wa kimataifa (ICASA2019) wa siku tano unaozungumzia masuala ya ukimwi na magonjwa ya zinaa Afrika. Mkutano huo umeanza jana Desemba 2 na unatarajiwa kumalizika Desemba 7 mwaka huu. 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Kigali. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amewataka viongozi barani Afrika kuwajibika kufanikisha malengo yaliyowekwa duniani  kutokomeza Virusi vya Ukimwi (VVU) ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 3, 2019 katika ufunguzi wa  mkutano wa 20 wa kimataifa wa siku tano kuhusu Ukimwi na magonjwa ya zinaa Afrika (ICASA), Dk Tedros amesema bado mamilioni ya walioathirika barani humo hawapo kwenye matibabu.

Kupitia mkutano huo unaofanyika kwa mara ya kwanza Afrika, Dk Tedros ameyataja mambo matatu ambayo viongozi wanatakiwa kuyazingatia wakati wa utekelezaji wa agizo hilo kuwa ni ugunduzi, masuala ya kijamii na uongozi wa kisiasa.

“Mapambano haya yameanza kwa miongo sasa, takwimu zinaonyesha mwaka 2018 watu milioni 1.7 walipata maambukizi mapya lakini mpaka sasa bado mamilioni ya watu Afrika hawapo kwenye matibabu,” amesema.

Amebainisha kuwa kundi linalopata maambukizi mapya kwa sasa ni wapenzi wa jinsia moja, wanaofanya biashara ya ngono, wanaojidunga dawa za kulevya na wafungwa. Amesema kundi jipya lililoingia ni vijana waliobalehe wenye umri wa miaka 15 hadi 24, kwamba wasichana wameathirika kwa kiwango cha juu.

Amewataka viongozi hao kuhakikisha wanawekeza fedha za ndani kuhudumia afya ili kuwezesha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba.

Advertisement

“Mpaka Desemba mwaka 2018 takwimu zinaonyesha watu milioni 77.9 milioni duniani wanaishi na VVU lakini mpaka sasa ni asilimia 80 ya walioathirika wanajua hali zao, asilimia 60 wameshaanza matibabu na ni asilimia 50 ambao wamefanikiwa kufubaza makali ya virusi,” amesema.

Akizindua mkutano huo, Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema wakati nchi yake ikifanikiwa kufikia malengo, viongozi wa kisera wajifunze kupitia mambo matatu.

“Kwanza Serikali ihakikishe inawekeza fedha nyingi katika afya, kuhakikisha inawafikia walengwa na wao kukubali hali zao, kuondoa unyanyapaa miongoni mwa jamii, kuondoa mila na desturi kandamizi na kuhakikisha matibabu ya mapema kwa walengwa,” amesema Kagame.

Awali Waziri wa Afya nchini Rwanda, Dk Diane Gashumba amesema nchi hiyo imefanikiwa kutokana na juhudi za ndani pamoja na kushirikiana ipasavyo na mashirika ya kimataifa.

Amesema nchini humo asilimia 99 ya wajawazito wamepimwa, asilimia 99 ya watoto walioathirika wapo kwenye matibabu.

“Asilimia 90 ya wanaoishi wa VVU wanajua hali zao kiafya, asilimia 98 yao tayari wapo kwenye mfumo wa matibabu huku asilimia 90 wamefanikiwa kufubaza makali ya virusi,” amesema Dk Gashumba..

Advertisement