Watoto 200 Tanzania kusailiwa ili kuigiza tamthiliya

Muktasari:

Watoto 200 wanatarajiwa kusailiwa kwa ajili ya kuigiza tamthiliya na Kampuni ya kutengeneza filamu ya J-Film 4 life


Dar es Salaam. Kampuni ya kutengeneza filamu ya J-Film 4 life imejitosa kuibua vipaji vya watoto  watakaoigiza tamthiliya mpya inayohusu watoto.

Idadi ya watoto wanaohitajika ni 200 wenye umri kuanzia    miaka minne hadi 14.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Septemba 2, 2019 na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Jeniffer Kyaka maarufu Odama alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa utafutaji wa vipaji vya watoto hao ambapo kilele chake kitakuwa  Septemba 14.

"Watoto wenye vipaji watakaopatikana watashiriki kwenye tamthilia inayowahusu ambayo kampuni yangu itaiandaa hivi karibu," amesema Odama.

Amebainisha katika usaili huo wanatarajia watoto zaidi ya 500 kushiriki huku wao wakihitaji 200 kati yao.

"Moja ya kundi kubwa katika jamii yetu ni watoto na sote tunatambua kazi ya sanaa ni kuelimisha na kuburudisha hivyo kwa kuibua vipaji tunaamini ni fursa kubwa kwa watoto kupata pa kutokea," amesema Odama.

Ameeleza tamthiliya wanayoenda kuitengeneza itaeleza maisha ya watoto katika mambo mbalimbali ikiwemo elimu, afya, migogoro ya familia kwa inavyowaathiri, dini, mirathi, tamaduni na mila.

"Aidha siku hiyo pia tumealika washirika mbalimbali wanaohusika na masuala ya watoto zikiwemo taasisi za elimu na mashule hivyo wazazi wasichezee nafasi hii katika kuwaleta watoto wao kwa kuwa naamini watakavyokuja sivyo watakavyoondoka," amesema.

Mwigizaji Jimmy Mafufu ambaye atakuwa mmoja wa majaji katika usaili huo amesema kwa watoto watakaopita katika mchujo wazazi wao wataingia mkataba wa kufanya kazi na Kampuni ya J-film 4 life kwa kuwa kisheria kwa umri wao hawaruhusiwi kufanya hivyo.

Kwa upande wake, mwigizaji mkongwe  Hashim Kambi ameipongeza kampuni hiyo kwa kuhusisha watoto wadogo, ambapo amesema itasaidia kuzalisha zao jipya katika tasnia hiyo na kuwa na wasanii ambao wamepitia mikononi mwa watu wenye uzoefu huo.