Waziri Kabudi aipongeza Airtel kwa kuzindua huduma za kifedha Afrika Mashariki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akimkaribisha ofisini kwake Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Sunil Colaso ambaye alimpa taarifa kuhusu huduma mpya ya kulipia kwa Airtel Money kwa nchi za Afrika Mashariki. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi  leo Jumapili Septemba 22, ameipongeza Airtel Tanzania kwa  kuanzisha huduma ya pamoja ya kutuma na kupokea pesa kupitia Airtel Money kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.

Waziri Kabudi alitoa pongezi hizo ofisini kwake wakati akipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Bw Suni Colaso Kuhusu huduma mpya za Airtel Money  ambapo watumiaji wa huduma ya Airtel Money kutoka nchi hizo sasa wanaweza kufanya malipo katika nchi tajwa kwa kutumia simu zao wakiwa popote kwani huduma hii imeshazinduliwa tayari.

“Ushirikiano huu kati ya Airtel Tanzania na watoa huduma wengine wa Airtel kutoka Kenya, Uganda na Rwanda utasaidia kukuza biashara kati ya nchi hizo nne kwani itakuwa rahisi kutuma na kupokea pesa, kulipia bidhaa au huduma mbalimbali kwa kupitia huduma hii ya pamoja ya Airtel Money,” alisema.

Kwa mujibu wa Waziri Kabudi, wafanya biashara sasa hawatalazimika tena kubeba fedha nyingi mifukoni wanaposafiri katika nchi hizi na pia ujumbe wanaopokea baada ya kutuma pesa ni ushahidi tosha wa malipo kwa kupitia Airtel Money.

“Sisi kama Serikali tunaunga mkono hatua hii ya Airtel kwa sababu itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara katia ya nchi hizi za Afrika mashariki na pia  kuendeleza ushirikiano mzuri ambao upo baina ya nchi hizi,” alisema huku akitoa wito kwa Watanzania watumie huduma hiyo kwa wingi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Bw, Sunil Colaso alisema wao wanaamini uanzishwaji wa njia hii ya malipo na utumaji fedha katika nchi hizi za Afrika Mashariki utarahisisha biashara baina ya wananchi  wa mataifa haya na kuifanya hii iwe ni njia ya kipekee ya malipo kati ya nchi na nchi nyingine.

“Huduma hii pia ni nafuu kwani ada au malipo yake ni nafuu mno ikilinganishwa na huduma nyingine za fedha kimataifa,” alimuambia Waziri.

Alisema kwa sasa wateja wa Airtel Money wanaweza kupokea fedha moja kwa moja kwenye simu zao kutoka mitandao mingine ya Airtel kutoka Zambia na Malawi na watoa huduma wengine duniani ikiwemo Qatar, Oman, Afrika Kusini, Uingereza, Ushelisheli na UAE.