Waziri Nditiye asema hekima itatumika usajili wa laini kwa wasio na vitambulisho vya Taifa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye

Muktasari:

Kesho Jumatatu Januari 20, 2020 laini zote za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole zitazimwa. Ili uweze kusajili laini ni lazima uwe na kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho hicho.

Kigoma. Serikali ya Tanzania imesema itatumia hekima kuwasaidia wananchi walioshindwa kusajili laini za simu kwa sababu ya kukosa kitambulisho cha Taifa na namba licha ya kuanza mchakato wa kupata kitambulisho hicho.

Imesema wananchi hao taarifa zao zipo katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), huenda wamekosa kitambulisho au namba kwa sababu  zilizo nje ya uwezo wao.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Januari 19, 2020 na naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye katika mkutano wa ndani wa CCM mkoani Kigoma.

"Serikali itaona jinsi ya kutumia hekima kwa wananchi ambao taarifa zao zipo katika ofisi za Nida kuona namna ya kufanya lakini kwa wengine ambao hawajajaza fomu laini zao zitazimwa,” amesema Nditiye.

Amesema ambao laini zao zitazimwa ni wale waliosajili laini chache na kuacha nyingine licha ya kuwa na kitambulisho hicho.

Amebainisha kuwa usajili wa laini za simu ni endelevu licha ya baadhi ya wananchi kupuuza.

Kesho Jumatatu Januari 20, 2020 laini zote za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole zitazimwa. Ili uweze kusajili laini ni lazima uwe na kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho hicho.