Zanzibar yamzungumzia mtalii aliyekufa maji akimchumbia mpenzi wake

Sunday September 22 2019

 

By Haji Mtumwa, Mwananchi

Unguja.  Mwili wa Steven Weber, aliyekufa maji  akiwa anamchumbia mpenzi wake, Kenesha Antoine  umechukuliwa na ubalozi wa Marekani kwa ajili ya uchunguzi.

Weber na Kenesha walipanga chumba kilichozungukwa na vioo kilichopo chini ya maji katika hoteli moja kisiwani Pemba.

Mtalii huyo anadaiwa kufa maji wakati akiogelea kutoka chini ya bahari usawa wa chumba hicho alikokwenda kumuonyesha mpenzi wake ujumbe wa mapenzi aliomuandikia pamoja na pete kupitia kioo ambacho mtu aliyeko chumbani anaweza kushuhudia kila kitu kinachoendelea chini ya maji.

Karatasi yenye ujumbe huo ilisomeka: “Siwezi kuzuia pumzi zangu kwa muda mrefuili kukwambia kila kitu ninachokipenda kwako, lakini kila kitu ninachokipanda kwako nakupendea zaidi kila siku.”

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Septemba 22, 2019, katibu mtendaji kamisheni ya utalii Zanzibar, Abdalla Mohamed amesema  taarifa kutoka kituo cha Konde, Pemba zinaeleza mtalii huyo alifariki akiwa anaogelea.

Amesema mwili wa Weber umechukuliwa na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa ajili ya uchunguzi na mazishi.

Advertisement

"Kwa sasa sina mengi ya kusema kuhusu hili. Maiti  imeshachukuliana, Jeshi la Polisi Zanzibar  wanaendelea kufanya uchunguzi kuhusu tukio hili," amesema.

Advertisement