Zitto awasha moto bungeni Tanzania

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe amesema Serikali ya Tanzania imewasikiliza Benki ya Dunia (WB) kwa kufuta na kurekebisha baadhi ya vifungu katika Sheria ya Takwimu baada ya benki hiyo kuzuia dola za Marekani bilioni 1.15.

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo) Zitto Kabwe amesema Serikali ya Tanzania imewasikiliza Benki ya Dunia (WB) kwa kuleta marekebisho ya Sheria ya Takwimu baada ya kuzuia Dola za Marekani bilioni 1.15.

Zitto ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 27, 2019  wakati akichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 3 wa mwaka 2019.

Amesema kwa mara nyingine katika Bunge hilo la Tanzania imepelekwa sheria ambayo inakwenda kuminya uhuru wa Watanzania.

Zitto  ambaye ni Kiongozi wa ACT- Wazalendo, amesema walianza na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya vikokotoo vya pesheni na haki za wafanyakazi .

“Huu ni mwendelezo wa sheria wa kukandamiza Watanzania. Ni bahati mbaya kuwa wananchi walio wengi ni masikini sana wakizungumza na hata wabunge wao wakizungumza hayasikilizwi,” amesema.

Amesema walizungumza kuhusu kifungu 24 A na B cha Sheria ya Takwimu kuwa kinaleta matatizo makubwa ya kunyima haki za watu lakini hawakusikilizwa.

Hata hivyo, amesema juzi Benki ya Dunia ilizuia fedha Dola za Marekani  bilioni 1.15 wamesikilizwa.

Zitto alisema Serikali ya awamu ya tano imekubali jambo ambalo wananchi na wapinzani walilipigia kelele lakini hawakusikilizwa.

Amesema sheria hiyo imebadilishwa leo hata mwaka haijatimiza na kwamba watu wale wale wanasimama na kuiambia Serikali kuwa ni sikivu.

“Wala tusihangaike na Takwimu nina barua kutoka Ikulu na Wizara ya Fedha kumuomba Rais aruhusu kabla ya mkutano huu wa Bunge Sheria ya Takwimu irekebishwe na mmetii mmeileta imerekebishwa, mnawasikiliza zaidi mabeberu kuliko wananchi wenu walioikataa sheria hii,” amesema.

Aidha, amesema Serikali ya Tanzania inafanya marekebisho Sheria ya Makampuni ikiwemo kukifanyia marekebisho tafsiri ya neno kampuni.

Amesema nchi zote za Jumuiya ya Madola zinatafsiri moja ya neno kampuni.

“Inaenda kuunganisha kampuni na mwenye kampuni kuwa kitu kimoja, jambo ambalo tutachekwa duniani na hakuna mtu atakayekuja nchi hii kuwekeza fedha zake ili kutengeneza ajira, ili kulipa kodi,” amesema.

Amesema yeye anafahamu marekebisho hayo yameletwa kwa sababu Serikali inahangaika na Kampuni ya Acacia.

Ameitaka Serikali kwenda kupambana na kampuni hiyo kwa utaratibu wa kiutawala badala ya kuharibu nchi kwa ugomvi wa kampuni moja.

“Kwanini mnatutia aibu duniani kwa kuleta sheria za ovyoovyo namna hii, kwa nini halafu mnampa wizara kijana smart inno kwenda kuhangaika na mambo ya kijinga kijinga kama haya,” amesema.

Hata hivyo, Mnadhimu Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni, Jenista Mhagama amesema hawawezi kukubali maneno kama hayo ya kuudhi na kudhalilisha na kwamba hayakubaliki.

Amemtaka Zitto kurekebisha maneno hayo na kutumia utaalam wake kuishauri Serikali.