‘Tulisota wiki nzima kumuona P Funk Majani’

Akiwa kidato cha pili, Domokaya anasema alirekodi wimbo akiwa na rafiki yake, Furaha Haleluya, hiyo ilikuwa ni kabla ya kukutana na Mandojo, wimbo ambao ulimpa misukosuko shuleni.

“Tulitoa singo yetu wakati huo, japo haikuvuma sana, lakini kwa pale Arusha ilitikisa, nakumbuka niliitwa kuhojiwa redio Clouds walikuwa na tawi kule Arusha, mtangazaji alikuwa Vivian (sasa ni marehemu),” anasema.Anasema harakati za kwenda kurekodi huo wimbo ulisababisha watimuliwe shule yeye na rafiki yake Furaha

“Wakati tunasoma, nilikuwa na rafiki yangu mwingine anaitwa Shujaa, huyu kutoa elfu 30 kukupa ukafanye kitu alikuwa haoni shida, sijui alikuwa anapata wapi, alitusadia pesa tukaenda studio kurekodi.

“Wakati huo tuko kidato cha pili, hivyo tukawa tukimaliza ratiba za shule, tunaenda studio, siku moja ilikuwa ni ya michezo, tukaambiwa turudi nyumbani kufuata vifaa.

“Sisi tukaitumia ile nafasi kwenda studio, tukiwa na sare za shule, kule mjini tukakutana mkuu wa shule, Furaha ndiye alimuona akakimbia, mimi naye nikakimbia lakini sikujua nakimbia nini, baadaye namuuliza vipi? Ananiambia kwani hujamuona headmaster?.

“Licha ya kukimbia kumbe alituona, ingawa tulifanya ujinga kukimbia, tungesimama na kujitetea kuwa tunakwenda kufuata vifaa, lakini tayari tulionekana kama tumetoroka shule, aliandika majina yetu kwenye karatasi , siku iliyofuata tulisimamishwa shule mwezi mmoja

“Tukiwa tunatumikia adhabu, siku moja tulienda shule, tuliwakumbuka tu wanafunzi wenzetu tukaona tupite, tukaambiwa tunataka kuchoma shule, tukatulia hadi tulipomaliza adhabu tukarudi kuendelea na masomo, haikutusumbua kwa sababu pamoja na kupenda muziki tulikuwa na akili darasani.

“Tulikuwa tukipewa nafasi ya kuigiza au kupafomu kwenye mahafali, tulifanya kweli, hii kidogo ikatupa unafuu na kuna makosa mengine madogomadogo tulisamehewa kutokana na kutoa shoo ya nguvu kwenye mahafali baadhi ya walimu na wanafunzi wakawa wanatukubali,” anasema Domokaya.

Anasema adhabu aliyopewa shule haikuleta shida sana nyumbani, kwani alipojieleza kuwa yupo kwenye harakati za kutimiza ndoto zake za muziki mama yake alimuelewa kwa sababu alikuwa na ratiba ya kujisomea na kufanya vizuri kwenye masomo.

“Mazoezi ya muziki, kuimba na kuandika nyimbo nilifanya usiku sana wakati wao wamelala, kidogo hii pia ikanibeba kwa wazazi niliposimamishwa shuleni ikaonekana ni bahati mbaya kwa kuwa sikuwa na tabia ya kutoroka shule wala kutojisomea,”.

Shoo ya kwanza apewa zawadi soksi

Katika harakati zake za muziki, Domokaya anasema yeye na Furaha walikuwa na tabia ya kuomba kupafomu kwenye matamasha ya Bongofleva jijini Arusha siku za mwishoni mwa wiki.

“Ili kupata nafasi ilikuwa kuna mchujo, wale bora ndiyo wanapewa nafasi ya kupafomu mwanzo mwanzo kwenye matamasha, ingawa wakati mwingine tukisikia kuna tamasha sehemu fulani, tunaenda kwa DJ tukiwa na CD za beats za Ulaya, tunamwambia sisi ni wasanii, tunaomba kupafomu, huo ndio ulikuwa utaratibu wetu.

“Nakumbuka kuna tamasha moja lilishindanisha makundi kama 50 hivi, mimi na Furaha pia tukaenda kama kundi, tukachana na kumaliza kwenye nafasi ya tatu,”.

Anasema walipewa zawadi ya soksi na Sh30,000 ambayo waligawana nusu kwa nusu, ingawa baada ya hapo hakurudi tena jukwaani kwenye matamasha hadi alipokuja kufanya kazi ya Nikupe na Mandojo.

“Niliona kama najishusha, nilikuwa na kipaji, lakini nikawa naona sipati fursa ipasavyo, wakati mwingine DJ anakubania, nikasema kwenye matamasha mimi tena basi, nikaweka lengo la kurudi jukwaani na wimbo, katika harakati hizo ndipo nikakutana na Mandojo hadi tukaja kutoa wimbo wa Nikupe,”.

Afanya Nikupe akiwa kidato cha nne

Akiwa kidato cha nne, Domokaya anasema ndipo aliandika wimbo wa Nikupe, akiwa na Mandojo ambaye alikuja kuwa kaka na rafiki yake mkubwa kushinda hata Furaha ambaye walianza harakati za muziki pamoja shuleni.

Anasema waliandika mashairi ya wimbo huo kwa hisia tu akiwa na Mandojo na kuanza kuimba kabla ya kuuingiza kwenye gitaa hadi walipokutanishwa na P Funky Majani aliyewapa fursa ya kwenda Dar es Salaam kurekodi.

“Tulipokuja Dar tukafikia kwa baba mdogo Kiki, Vingunguti, tukaibiwa kila kitu, baba mdogo Mwenyezi Mungu amrehemu, alinipa kisuruali kinjiwa (fupi) cha kitambaa na malapa, ndiyo nilikwenda navyo studio.

“Wakati ule ilikuwa hadi kuonana na Majani kufanya naye kazi ni shughuli, sisi alitwambia twende Alhamisi, ile tumefika hata geti hatukufunguliwa, tuliishia nje, msaidizi wake alifungua kidirisha akatuchungulia na kutwambia zamu yenu kesho sio leo akafunga.

“Siku iliyofuatia tukaenda ikawa ni yaleyale, ilituchukua wiki nzima hadi kufunguliwa geti kuingia ndani, kama sio Mandojo mimi nilishakata tamaa, kuna wakati nilimueleza kwamba narudi zangu Arusha, kurekodi tena basi.

“Dojo alinisihi sana, akaniambia mdogo wangu vumilia, maisha ni kupambana, nakumbuka nyumbani napo nilikuwa kama nimepotea natafutwa, nikahisi labda sijapata baraka za mama ndiyo sababu yote yanatokea, ukiangalia tumefika tu na kuibiwa kila kitu, lakini kwa Majani pia mambo hayaendi, kama sio Dojo mimi ningeondoka, lakini baada ya wiki tukafanikiwa kurekodi na kurudi Arusha.

“Tuliendelea kumpigia simu mara kwa mara tukiwa Arusha wakati huo tukijitambulisha kama madogo wa gitaa, kumuulizia vipi kazi yetu, alitwambia tuvumilie kwani anataka kuifanyia kazi kubwa ngoma yetu, tukawa wapole.

“Ilichukua muda mrefu sana, hadi tulikata tamaa, nilifanya mitihani yangu ya mwisho ya kidato cha nne na kujikita moja kwa moja kwenye muziki, ndipo tukaja kusikia ngoma inapigwa kila mahali Dar es Salaam, sisi hata hatuji ndipo tukaamua kuja jijini kusaka mkwanja wa kazi yetu.

Itaendelea kesho, Domokaya akieleza namna alivyofanya biashara ya viatu na Mandojo kabla ya kujiingiza kwenye kilimo.