Abdul Writer: ‘Kombolela’, ‘Mama Kimbo’ Akili nyingi ya uandishi

“Niliitwa na mkuu wa Idara, Dk Chacha, wakati huo taarifa zimeanza kusambaa kuwa nimeandika barua ya kuacha chuo, nilianza kuacha kuingia darasani, wengi walishangaa naacha boom (mkopo) na kila kitu, narudi mtaani. “Kilikuwa ni kipindi kigumu kwangu kueleweka, ingawa hata mimi sikujua narudi mtaani kufanya nini, lakini sikutaka tena kuendelea na shahada yangu ya kwanza ya sheria," anaanza kueleza Abdul ‘Writer’ Juma katika mahojiano maalumu na Mwananchi.

Mtayarishaji na mwandishi huyo wa mwongozo wa filamu, tamthilia na vipindi nchini ambaye mkono wake umehusika kwenye uandishi wa tamthilia maarufu, zikiwamo ‘Saluni ya mama Kimbo’, ‘Kombolela’ na ‘Zahanati ya kijiji’ anasema familia yake iliamini fani ya sheria ni bora zaidi, japo kwake ilikuwa kinyume.

"Nilipohitimu kidato cha sita, mwaka 2013 nilidahiliwa kama mwanafunzi wa sheria Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), tena niliyepata mkopo na kuanza chuo, lakini kama kijana niliyelelewa na mama, baba yangu alifariki nikiwa na miaka mitano, nilihisi safari yangu itakuwa ndefu sana kwenye kozi hiyo, niliamini nahitaji kusomea kitu ambacho sitokaa darasani miaka mingi zaidi.

"Niliwaza, kwenye sheria natakiwa kusoma miaka minne, nikitoka pale niende law school (shule ya sheria), sijui huko nitamaliza lini, ukijumlisha na akili za ujana za kutaka kujaribu kufanya vitu vingine, nikaona sitaweza kusoma miaka yote hiyo, tayari nilikuwa nimesoma muhula mmoja pale UDOM, nikaandika barua ya kuacha chuo.”
Anasema hakuna aliyeamini kama anaacha chuo, hata walimu walihisi anahitaji msaada wa kisaikolojia kwa kuwa aliomba kuacha chuo kipindi ambacho anafanya vizuri darasani, hivyo uamuzi wake ulitafsiriwa kuwa ni wa kijinga kuwahi kutokea.
"Niliandika ile barua bila kuishirikisha familia yangu, wakati huo tulikuwa tumefanya jaribio, tukikaribia kufanya UE, Dk Chacha alikuwa ameingia darasani kurudisha matokeo ya jaribio tulilofanya na nilikuwa nimepata 13/15, akauliza huyu mtu yuko wapi?

"Alimwambia mwanafunzi mmoja ambaye nilisoma naye sekondari Azania, mimi nikaenda kidato cha tano na sita Makumila, Arusha nikaja kukutana naye UDOM na tukawa tunaishi pamoja, asimuone darasani kesho yake hadi awe na mimi.

"Tulipokwenda shule Dk akaniangalia akaniuliza kwa nini sihudhurii vipindi, nikamwambia niko kwenye harakati za kacha chuo, akaniambia kesho asubuhi tukutane ofisini kwake, nilikwenda akanikutanisha na mkuu wa idara ya sosholojia, niliwekwa kikao ambapo nilieleza msimamo wangu.

"Wakaomba namba ya mama ili aelezwe kuhusu hilo lakini sikuwapa. Nilisemwa sana, niliporudi hosteli nikamuandikia mama meseji ndefu sana, sikusubiri majibu yake nikazima simu, siku iliyofuatia niliondoka kurudi nyumbani.

Anasema ilikuwa ni ngumu kupokelewa na familia yake, mama yake alimueleza hataki kuomuona nyumbani, alimpa muda hadi kufikia Oktoba atafute pa kwenda kwani hawezi kuishi na watu wasiotaka kusoma.

"Niliishi nyumbani kama mgeni, nilikuwa nikisikia mama amerudi nakwenda kujificha, maisha yangu yalikuwa ni ya ndani tu, sikutoka, ingawa mipango yangu ilikuwa mwaka 2014 niombe upya chuo, lakini kozi ambayo sitosoma miaka mingi.

"Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) waliniambia ili niweze kuomba, lazima nirudishe asilimia 25 ya mkopo wa muhula mmoja ambao nilipewa zaidi ya Sh milioni 2, hivyo nilipaswa kurejesha kama laki tano na kidogo, nazipata wapi sijui na mama hakutaka hata kunisikiliza, ikabidi nijiongeze, ambapo nilitafuta kazi ya ualimu wa kujitolea.
 

Ajikita kwenye ualimu shule za kata

Anasema baada ya kusota nyumbani, haeleweki, aliamua kuomba kibarua cha kufundisha moja ya sekondari katika shule za kata huko Mbagala.
"Mkuu wa shule alinikubalia kwa malipo ya Sh 150,000 kwa mwezi, nikaanza kufundisha, hata hivyo kuna wakati pesa haitoshi kwa mwezi unapewa Sh80,000 huwezi kuiacha, katika harakati hizo nikaanza kuipenda kazi ya ualimu.

"Nilianza kujifunza vitu vingi kwa walimu wenzangu pale shuleni, maisha yao, maadili ya kazi na mambo mengine ya walimu, nikajikuta tu naipenda ile kazi kwa moyo wangu wote.

"Kwa kuwa mshahara ulikuwa ni mdogo, nikaanza kuishi kwa madili, kuna muda tukawa na mitihani ya ndani ya Jumamosi, nikapata wanafunzi kibao.
"Ili kupunguza gharama, nikatafuta sehemu ya kutolea kopi ya picha ya bei rahisi ambapo nilikuwa ninatoa kwa Sh50 kule Kariakoo, ili tu kupata faida, nilipata wanafunzi wa kidato cha pili kama kama 400 kila mmoja analipia Sh500, nikawa najibana hivyohivyo maisha yanaenda.

"Kifupi niilipenda kazi ya ualimu, japo wakati huo bado hatukuwa tukielewana vizuri na mama, lakini alivyokuwa akiniona napambana, nikirudi nyumbani jioni niko bize nasahihisha mitihani, kama mzazi akaanza kunionea huruma.

"Ilipofika kipindi cha udahili, tayari nilishapata pesa ya kurudisha TCU, ile ya mkopo niliyopewa nilipokuwa UDOM, kama taratibu zilivyonitaka niilipe asilimia 25 ndipo niombe upya chuo.

"Wakati natoka Dodoma, watu walinitafsiri kama sitaki chuo au masomo kwa ujumla, lakini nilitaka kitu ambacho kitanilipa kwa muda mfupi, hivyo mipango yangu ilikuwa nilirudi mwaka unaofuatia lakini kwenye kozi nyingine.
"Katika kile kipindi cha kusubiri wakati najitolea kwenye ile shule ya kata, nikajikuta naupenda kwa dhati ualimu, nilipata uzoefu wa namna wanavyosimama na maisha yao.

"Hivyo niliporudi chuo nikaomba kusoma shahada ya kwanza ya ualimu, nilipofanya hivyo kwa mara nyingine nilionekana kama kichaa, kila aliyenifahamu aliniambia kwa nini umeacha sheria, unaenda kwenye ualimu? "Hata mama aliniambia babu yako alikuwa mwalimu na hadi anafariki amekufa maskini, kinachokupeleka huko wewe ni nini? Watu walinishangaa, wapo walionishauri nisome meneja rasilimali watu, utawala, lakini nikasema nitakwenda kuwa mwalimu wa tofauti," anasema.

Anasema aliamini atakuja kuwa mwalimu fulani mwenye maendeleo, alipangiwa chuo Kikuu cha St Augostino tawi la Iringa, na hapo ndipo safari yake rasmi kwenye ualimu ikaanza. "Nilipofika tulitakiwa kujaza masomo ambayo kila mmoja ataweza kuwa nayo huru kufundisha darasani, tulikuwa wengi kama walimu 600, tulidahiliwa lengo ilikuwa nifanye HGL, katika kujaza masomo nikajiuliza nijaze histori au literature, mtu akatokea tu akanishauri nifanye literature.

"Ajabu kati ya walimu 600 waliodahiliwa, darasa letu literature lilikuwa na walimu 40, wengi walijaza history, jiografia na Kiswahili, nilihofu kwenye literature, lakini nikasema mbona sheria ilikuwa ni zaidi ya hii nitaweza na kuanzia pale nikawa na hamasa ya kutaka kufanya kitu,” anasema.

Anasema akiwa anasoma shahada ya ualimu, ndipo alianza kuandika tamthilia na filamu na aliifanya hiyo kazi kwa mapenzi na ubunifu.
"Japo nilikuwa napenda sana kutazamana filamu na tamthilia za Nigeria na za hapa nyumbani nikiwa mdogo, lakini kule kwenye literature ndipo nilipata hamasa nyingine ya kuandika.

"Sikuwa na jina, hivyo kazi zangu zilionekana kama kitu cha kawaida, kutokana na ukweli kwamba hapa nyumbani wengi wanamuangalia nani ana jina na sio nani amefanya nini?

"Niliendelea kuandika hadi nilipohitimu chuo, wakati huo ilikuwa ni 2017, nilikuwa tayari nipangiwe kokote kule nikafundishe, nilipenda ualimu kutoka moyoni, bahati mbaya ajira za Serikali zilikuwa ngumu. "Hata hivyo tayari nilishaanza kufahamiana na wasanii baadhi, akiwamo kaka yangu Single Mtambalike (Richie Richie) ambaye alinisaidia nikapata ajira kwenye shule moja kubwa binafsi jijini Dar es Salaam yenye madarasa ya msingi na sekondari.
 

Aandika barua ya kuacha kazi

"Ni uamuzi mwingine mgumu ambao niliufanya, nikiwa mwalimu, niliendelea kujaribu kugonga milango ya sanaa bila mafanikio, ilikuwa haifunguki, kuna muda nilikataliwa hadharani, lakini nilizidi kujipa moyo.

Abdul Writer anasema ratiba ya ualimu ilimbana na kutaka kumtoa kwenye ramani ya sanaa, kwani alifundisha madarasa tofauti ya msingi, kidato cha nne na cha sita
"Mwenye shule pamoja na kwamba nilifanya kazi na somo langu watoto walifanya vizuri, lakini alitaka kuniona kazini muda wote, jambo ambalo lilikuwa ngumu kujigawa na kupata muda wa sanaa, kuna muda unaondoka unamuomba mwalimu mwenzako akushikie kipindi chako, wewe utalipa kesho yake.

"Nilisemwa sana na kulamba memo nyingi, lakini walishindwa kunipa adhabu kubwa kutokana na maendeleo ya madarasa niliyokuwa nafundisha, hakuna mtoto aliyepata chini ya 65 ambao ndio ulikuwa wastani wa chini wa shule, ingawa ratiba ilizidi kuwa ngumu.

"Nilikuwa nafundisha madarasa ya mitihani, naishi Mbagala na shule ipo Tabata, saa 12 asubuhi unatakiwa kuwa darasani, kutoka ni saa 3 usiku, kisha niende kwenye sanaa, sikuwa napata muda wa kulala, wakati mwingine nafika nyumbani saa 8 usiku.

Hata familia pia ilikuwa inanisema, lakini yote ilikuwa ni sababu ya kutaka kuonyesha nilichonacho kwenye sanaa. "Siku moja nilimpeleka babu hospitali, nikawa nimechelewa kama dakika 10 hivi kufika kazini, nilifokewa mno na mwalimu mkuu wa taaluma lakini ni kipindi ambacho nilikuwa na wazo la kuacha kazi ili nijikite kwenye sanaa, japo nilikuwa na hofu nikifanya hivyo nini kitatokea.

"Aliniambia kama vipi acha kazi ya ualimu ambayo nilikuwa nimeshaitumikia kwa miaka mitatu, wakati huo kuna wanafunzi wenzangu niliosoma nao hawajapata ajira na ni walimu wazuri, wengine wananifuata getini kazini kwangu wanaomba niwasaidie, lakini mimi nataka kucha kazi? nilijiuliza.

Lakini siku hiyo nilikwenda kumwambia Ofisa rasilimali watu kuwa nimeamua kuacha kazi, alistuka akasema hauko sawa? nikamwambia ndiyo, nikaandika barua hiyo ilikuwa 2020.

Anasema kipindi hicho, akaunti yake ilikuwa na Sh 150,000 tu, hakufahamu ataishije, lakini aliamini kipaji chake kitamuwezesha kuishi na kujitafuta kwa mara nyingine.
Kufahamu safari yake hadi kumshirikisha mama Kimbo kwenye tamthilia yake ya kwanza, alipomtoa Kimbembe na namna alivyomwaga chozi alipoambia arudie kufanya kazi upya ambayo alitumia pesa ya mkopo kuitengeneza? usikose gazeti la kesho.