Albamu za Bongo Fleva zilizobamba 2024

Muktasari:
- Mfumo wa usikilizaji wa kazi za wasanii kwa miaka ya hivi karibuni unategemea zaidi Digital Platform mbalimbali ambazo hutumiwa kama majukwaa ya kuwakutanisha mashabiki na kazi za wasanii wao pendwa
Dar es Salaam. Mwaka 2024 wasanii wa Bongo Fleva wameendelea kuachia albamu na Ep ikiwa kama sehemu ya kuendelea kujitanua kimuziki na kujitangaza zaidi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Mfumo wa usikilizaji wa kazi za wasanii kwa miaka ya hivi karibuni unategemea zaidi Digital Platform mbalimbali ambazo hutumiwa kama majukwaa ya kuwakutanisha mashabiki na kazi za wasanii wao pendwa.
Majukwaa hayo ya kusikilizia muziki kama Boomplay, Audiomack, Spotify, Apple Muziki na mengineyo yanaonesha idadi ya watu waliosikiliza kazi za wasanii hao. Licha ya kuwa mwaka huu zipo kazi nyingi zilizoachiwa lakini hizi ndizo albamu zilizofanya vizuri 2024.
Therapy ya kwake Jay Melody, ambayo ilitoka Aprili 25, 2024 ikiwa na jumla ya nyimbo 14, imefanikiwa kufikisha wasikilizaji milioni 12 kwenye mtandao wa Audiomack huku ikiongoza kukaa namba 1 kwa zaidi ya mwezi kwenye jukwaa hilo.

Lakini pia Therapy imefanikiwa kufikisha zaidi ya wasikilizaji milioni 51.3 kwenye Boomplay huku nyimbo kama Wa Pekeyangu, 18, zikifanikiwa kuingia katika orodha ya nyimbo ishirini bora kwenye jukwaa hilo.
Nipeni Maua Yangu kutoka kwa Roma Mkatoliki, iliyoachiwa rasmi Juni 6, 2024 ikiwa na jumla ya nyimbo 15 ni miongoni mwa albamu zilizofanya vizuri ikiwa na zaidi ya wasikilizaji 1,272,406 kwenye jukwaa la Audiomack ikifanikiwa kuongoza namba 1 kwa zaidi ya mwezi na mpaka sasa ipo nafasi ya 5 kwenye jukwaa hilo.
Pia albamu hiyo imefanikiwa kusikilizwa na watu milioni 10.5 kupitia mtandao wa Boomplay huku streams milioni 8 akiwapata ndani mwezi mmoja.

Albamu hiyo ilifanikiwa kuingiza ngoma zote 15 kwenye trend ya chart ya jukwaa hilo hii ilikuwa rekodi kubwa siyo tu kwa Roma lakini pia kwa muziki wa Hip-hop Tanzania.
The Gods Son kutoka kwa Marioo, ilitoka Novemba 29, 2024 ikiwa na jumla ya nyimbo 17, hii ni albamu ya pili kutoka kwa King Bad Marioo. Ya kwanza ni ile ya The Kid You Know iliyotoka 2022.
The Gods Son, imefanikiwa kuingia namba moja Audiomack Tanzania, ikiwa ni saa 24 baada ya kuachiwa kwake na imeendelea kukaa hapo mpaka sasa ikiwa na zaidi ya wasikilizaji 1,241,527 kwenye mtandao huo.

Albamu hiyo ambayo imeandaliwa na wazalishaji muziki kama vile Abba Process, S2kizzy na wengine ilifanikiwa kuingiza nyimbo 13 kwenye trend ya nyimbo 15 ya Apple music Tanzania.
Marioo akiwa amewashirikisha wasanii kama Harmonize, Patoranking, Kenny Sol, Bien n.k amefanikiwa kufikia wasikilizaji milioni 1.9 kwenye mtandao wa Boomplay kwa muda mfupi baada ya kuachiwa kwake.
Msanii Bora Wa HipHop ya kwake Stamina ambayo ilitoka Novemba 14, 2024 ikiwa ni kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwake. Msanii huyo aliamua kuwazawadia mashabiki albamu hiyo ikiwa na nyimbo 17 ambazo amewashirikisha wasanii kama Jay Rox, Belle 9, Wagosi Wa Kaya, Kusah, Linah, Mwasiti na wengine huku ikipikwa na watayarishaji Bear Beat, SMG, Bin Laden, Chiby, Papa, Dully Sykes n.k.
Albamu hiyo imefanikiwa kupata wasikilizaji 150,753 kwenye jukwaa la Audiomack na ipo nafasi ya 5 mpaka sasa kwa albamu zinazofanya vizuri Tanzania pia imefikisha streams zaidi ya 349,000 kwenye jukwaa la Boomplay.
Mbuzi kutoka kwa Young Lunya, ina jumla ya ngoma 11 zilizoipa heshima ya kusikilizwa na zaidi ya watu 1,432,441 kwenye mtandao wa Audiomack huku ikiendelea kubaki kwenye trend kwenye jukwaa hilo kwa zaidi ya miezi mitano tangu kuachiwa kwake.

Lunya amewashirikisha wasanii kama Khaligraph Jones (Kenya) kwenye wimbo wa Stupid, Dvoice (Tanzania) kwenye wimbo wa Mama Wee, Dutchavelli (England) na wengine wengi.
Peace and Money, ya kwake Zuchu ni kati ya albamu iliyotoka mwaka huu na kufanya vizuri. Albamu hiyo iliachiwa Desemba 20, 2024 ikiwa na jumla ya nyimbo 12 ambazo ni pamoja na Till I Die, Lollipo, Mwizi, Antenna, Makonzi na zingine nyingi.
Kwenye albamu hiyo Zuchu amefanikiwa kuwashirikisha wasanii wakubwa kutokea Afrika akiwemo Diamond Platnumz ambaye ameshirikiana naye kwenye wimbo wa Wale Wale, H_Art The Band kwenye Tinini, Yemi Alade kwenye Lollipop na Spyro kwenye Till I Die.

Album ya Peace And Money imepata mafanikio makubwa kwenye majukwaa mbalimbali ya kusikiliza muziki. Ndani ya siku tatu tangu kuachiwa kwake ilifanikiwa kushika namba moja kwenye nchi zaidi ya 20 duniani , kama Tanzania, Kenya, Oman, Comoros, Bulgaria, China katika mtandao wa Audiomack, huku ikifanikiwa kusikilizwa kwa zaidi ya mara 3,968,695 kwenye mtandao huo.
Peace And Money imefanikiwa kufikisha wasikilizaji Milioni 1.3 ndani ya siku tano tangu kutoka kwake kwenye jukwaa la Boomplay. Lakini pia ndio albamu namba moja kwenye mtandao wa Apple Muziki.
Hii ni albamu ya kwanza kwenye safari ya muziki wa Zuchu ambayo imetoka baada ya EP yake iliyotoka Aprili 13, 2020 ikiwa na nyimbo 7.
Maana ya albamu
Akizungumzia hilo, Frank Daxx ambaye amekuwa akitumia mitandao kueneza uelewa wa muziki, amesema kwa kawaida albamu, EP na mixtape zinatofautishwa kwa idadi ya nyimbo, dakika za nyimbo zote kwa ujumla na lengo kuu la kimaudhui.
Amesema albamu inatakiwa iwe na nyimbo kuanzia nane na kuendelea, muhimu zaidi inapaswa kuwa na mtiririko wa kimaudhui unaoshabihiana toka wimbo wa kwanza hadi mwisho.
Msikilizaji anakuwa kama anasoma kitabu kinachoelezea jambo fulani kuanzia ukurasa wa mwanzo hadi wa mwisho.
“Sasa wasanii wetu wanakusanya nyimbo zao kadhaa kali wanatoa anasema ni albamu, ukisikiliza hakuna muunganiko kati ya wimbo na wimbo, pia unakuta hakuna intro wala untro, maana intro anakuelezea hii albamu inazungumzia kipi hasa,” anasema Frank.
Naye mtayarishaji wa muziki na mmiliki wa Studio S.M.G Sampamba, amesema wasanii wengi wanaoachia EP na Albamu hawajui maana ya vitu hivyo.
“Ep maana yake ni Extended Playlist wenzetu Ulaya akikutengenezea Ep anakuwa ana mada ambayo anataka kuileta kwenye jamii ambayo inakuwa na nyimbo 3 mpaka 6 anaweza akaongelea mapenzi namna ambavyo alikutana na mpenzi wake mpaka kuachana hiyo ndiyo Ep lakini wasanii wetu hawafanyi hivyo.
“Albamu ni mkusanyiko wa mawazo kwa msanii inaweza kuwa maisha yake au chochote anachotaka kukizungumzia, mfano ukiangalia hata albamu ya picha watu wanaanza kuweka picha za zamani mwanzoni kisha za sasa zinafuata,” alisema Sampamba.